Wanafunzi 200,000 waacha shule Mwanza

Muktasari:

Takwimu zilitolewa na ofisa elimu Mkoa wa Mwanza, Martini Nkwabi, zinaeleza kuwa kati ya wanafunzi hao, 149,690 wa shule za msingi na 55,322 wa sekondari.

Mwanza. Wanafunzi zaidi ya 200,000 wa shule za msingi na sekondari, wameacha shule kwa vipindi tofauti kutokana na sababu mbalimbali mkoani hapa.

Takwimu zilitolewa na ofisa elimu Mkoa wa Mwanza, Martini Nkwabi, zinaeleza kuwa kati ya wanafunzi hao, 149,690 wa shule za msingi na 55,322 wa sekondari.

Nkwabi alisema hayo wakati akitoa taarifa ya hali ya elimu mkoani hapa kwenye kikao cha wadau wa elimu kilicholenga kujadili changamoto zinazoikabili elimu na kuzitafutia ufumbuzi ili kuongeza ufaulu.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mamlaka za serikali za mitaa zilizotolewa mwaka huu, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, wanafunzi wa shule za msingi waliosajiliwa walikuwa 158, 257 lakini waliomaliza walikuwa 312,545.

Mwaka 2016 hadi 2019, wanafunzi waliosajiliwa katika shule za sekondari walikuwa 158, 257 lakini waliomaliza ni 102, 935.

“Kuna sababu nyingi zinazofanya wanafunzi waache shule, hivyo tuna jambo hapa la kufanya maana ukiangalia hii namba ni kubwa mno kwa mkoa,” alisema Nkwabi.

Pia, alisema zipo sababu zinazofanya hali hiyo ikiwa ni pamoja na utoro, wanafunzi kupata mimba na ukosefu wa nidhamu kwa wanafunzi na walimu.

“Vyanzo vya utoro vipo kama vitatu, kwanza utoro unaweza kusababishwa nyumbani kama wazazi hawapo makini kufuatilia mienendo na kuweka msisitizo kwa watoto kwenda shule,” alisema Nkwabi.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali alisema licha ya kazi kubwa ya maofisa elimu kata ni kufuatilia maendelo na mienendo ya shule kwenye kata zao, lakini hawafanyi hivyo.

Bila kutaja takwimu, alisema wilaya yake inaongoza kwa wanafunzi kuwa na mimba.

“Hawa maofisa elimu kata hawatusaidii, kuna mwalimu mkuu wilayani kwangu amefanya mapenzi na wanafunzi wake zaidi ya watano na kuwapa mimba,,” alisema Kali.