Breaking News

VIDEO: Wasimamizi watakaovuruga uchaguzi kukiona

Sunday October 18 2020

By Yuvenal Theophil, Mwananchi

Moshi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema haitosita kumchukulia hatua za kisheria  msimamizi wa uchaguzi yeyote atakayefanya kwa makusudi vitendo vitakavyosababisha uchaguzi kuharibika katika jimbo au kata.
Makamu mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk  alisema hayo wakati akizungumza katika kikao kilichojumuisha waratibu na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha.

Manyara na Tanga iliyofanyika Mjini Moshi.
Mbarouk alisema kwa kuzingatia kifungu 89A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 88A cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura 292 vinavyowataka kutekeleza wajibu wao kutokana na mafunzo na maelekezo waliyopata kutoka Tume, kila mmoja asimame kikamilifu katika nafasi yake
“Ni matarajio ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa mafunzo na maelekezo iliyowapa yataleta matokeo chanya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 kwa kusimamia vyema vituo vya kupigia kura ili kuepusha lawama na uvunjifu wa amani,” alisema Jaji Mbarouk.

“Atakayesababisha matokeo ya uchaguzi kutenguliwa na Mahakama baada ya uchaguzi kwa kutozingatia  maelekezo ya tume na kuisababishia Serikali hasara ya kurudia uchaguzi atatakiwa kufidia hasara hiyo kwa mujibu wa kifungu 89B cha  sheria za uchaguzi serikali za mitaa sura 292,” alisema Jaji Mbarouk.

Pia, aliwataka wasimamizi hao ambao ni wakurugenzi  kuhakikisha wanahakiki vifaa vya uchaguzi vilivyoletwa kwenye maeneo yao ili kubaini kama kuna upungufu kabla ya siku ya kupigakura kwa lengo la kurahisisha zoezi hilo kwa wananchi waliojiandikisha ili wapate fursa ya kupiga kura.

Advertisement