Watoto 168 wazaliwa mkesha wa mwaka mpya 2020

Muuguzi hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro, Leila Shebila akimkabihdi kichaanga, Husna Ayub mkazi wa Ngerengere, aliyejifungua mtoto katika mkesha wa mwaka mpya 2020 ambapo jumla ya watoto tisa wamezaliwa huku kati yao wanaume saba na kike wawili. Picha na Juma Mtanda.

Dar es Salaam. Mkesha wa kuukaribisha mwaka 2020 umekuja na baraka ya watoto 168, waliozaliwa usiku wa kuamia jana katika zahanati, vituo vya afya na hospitali mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi jana, mganga mkuu mkoa wa Dar es Salaam, Dk Yudas Ndungile alisema takwimu zilizoingizwa kwenye mfumo watoto 168 walizaliwa.

“Mkoa wa Dar es Salaam takwimu tulizonazo watoto 168 wamezaliwa mkesha wa mwaka mpya kati yao, 81 ni wakiume na wakike 87,” alisema Dk Ndungile.

Waliozaliwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ni wawili.

Ofisa uhusiano wa MNH, John Stephen alisema: “Wamezaliwa watoto wawili wa kike na kiume. Wamezaliwa salama na afya zao ni nzuri mama na watoto.”

Kutoka mikoani

Katika mkesha huo watoto 13 walizaliwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC na Hospitali ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Kati yao watoto wanane wa kiume na watano wakike.

Ofisa uhusiano wa KCMC, Gabriel Chiseo alisema wanawake wanane walijifungua kwa njia ya upasuaji na wawili wakijifungua kawaida.

Pia, Chisseo alisema afya za watoto hao na wazazi wao zimeimarika na wanaendelea vizuri.

Katika hospitali ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, watoto watano wamezaliwa wa kike ni wawili.

Watoto 14 walizaliwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.

Mganga mfawidhi hospitali hiyo, Dk Majura Magafu alisema watoto hao waliozaliwa kwa njia ya kawaida ni wanane na upasuaji ni sita.

Dk Majura alifafanua kuwa kati yao wa kiume ni wanane hali zao na mama zao zinaendelea vizuri.

Pia, aliwataka wazazi kuzingatia ushauri wa kitaalamu waliopewa wa kunyonyesha watoto wao kwa miezi sita bila kuwapa kitu chochote na kuhakikisha wanahudhuria kliniki kila mwezi ili kujua maendeleo yao.

Kituo cha Afya Mirerani wilayani Simanjiro na hospitali ya wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, walizaliwa watoto sita kwenye mkesha huo.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Dk Malkiad Mbota alisema watoto wawili walizaliwa hospitali ya wilaya.

Dk Mbota alisema kati ya watoto hao wakiume na wakike hali zao ni nzuri na wazazi wao.

Naye mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Mirerani, Dk Hassan Ishabailu alisema watoto wanne walizaliwa.

Dk Ishabailu alisema kati ya watoto hao wawili ni wa kike na hali zao na mama zao wanaendelea vyema na wataruhusiwa wakati wowote.

Mmoja kati ya wazazi waliojifungua, Mariam Hussein alisema anafurahi kwa kuanza vyema mwaka kwa kupata mtoto wa kiume.

Kutoka mkoani Mwanza, ilielezwa watoto 22 walizaliwa katika Hospitali za Rufaa ya Bugando (BMC) na ya mkoa Sekou-Toure.

Kati ya watoto hao, wa kike ni 13 na wote walizaliwa kwa njia ya kawaida.

Msimamizi wa Hospitali ya SekouToure, Muyanji Nkumbi aliliambia Mwananchi kuwa watoto waliozaliwa hospitalini hapo ni 20 kati yao, 11 wakike.

Naye msimamizi wa zamu Hospitali ya Rufaa Bugando, David Dosa alisema katika mkesha huo walizaliwa watoto wawili wote wa kike.

Unicef yanena

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) nchini, linakadiria kuwa watoto 5,000 watazaliwa mwanzoni mwa mwaka mpya 2020 ikiwa ni miongoni mwa watoto 392,078 waliokadiriwa kuzaliwa duniani kote.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na mkuu wa kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa, Usiah Nkhoma alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa World Data Lab iliyochapishwa hivi karibuni na kitengo cha ongezeko la watu duniani cha Umoja wa Mataifa (UN).

Usiah alisema kila Januari, Unicef linasherehekea siku ya watoto waliozaliwa mwanzoni mwa mwaka.

Mwaka 2018, watoto wachanga milioni 2.5 walifariki dunia katika kipindi chao cha mwezi mmoja tangu wazaliwe.

Miongoni mwao, walifariki kutokana na matatizo ya kuzaliwa njiti, wakati wa kujifungua na maambukizi ya kifua, huku takwimu zikionyesha zaidi ya watoto 2.5 huzaliwa wamekufa.

Kwa Tanzania, watoto wana uwezekano wa kuepuka kifo wakiwa chini ya umri wa miaka mitano hivi sasa, ukilinganisha na miaka iliyopita.

Serikali imeimarisha huduma za mama na mtoto ikiwamo unyonyeshaji, chanjo, usambazaji vitamin A, kumlinda mtoto na Virusi vya Ukimwi (VVU) akiwa tumboni na kupambana na magonjwa yanayowashambulia watoto.

Ingawaje, Tanzania bado ni miongoni mwa nchi ambazo vifo vya watoto wachanga kuwa juu, kwa mujibu wa Unicef mwaka 2019 vifo 44,082 vilitokea baada ya kuishi chini ya siku 28 na wengine 76,644 walifariki kabla hawajatimiza mwaka mmoja.

“Tunachoangalia kwa sasa ni namna tutaondoa kabisa vifo vya watoto wachanga kwa kukinga hasa wanaofariki chini ya mwezi mmoja. Hivyo, wafanyakazi wa afya tuna jukumu la kulitimiza hili,” alisema Rene Van Dongen, mwakilishi mkazi wa Unicef nchini.

Imeandikwa na Herieth Makwetta (Dar), Joseph Lyimo (Manyara), Joyce Joliga (Songea), Janeth Joseph (Moshi) na Jesse Mikofu (Mwanza)