VIDEO: Waziri Kigwangalla adai kuna njama za kutaka kumuua

Thursday January 23 2020

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amekuwa maarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na ujumbe tata ambao huwa anaandika katika akaunti zake na kwa kiasi kikubwa kuibua mijadala.

Lakini ujumbe aliotoa katika siku za karibuni, si tata na unaoibua mijadala, bali umeacha wengi na mshangao kutokana na kuwa kada, nafasi katika jamii na wadhifa wake kama waziri.

Ameandika kuhusu kundi ambalo anasema linahaha kumchafua na hata kutaka “kumuua” na kuahidi kulipa kisasi kwa kila njia, huku akibainisha siri kadhaa za kunusuru maisha yake.

Vita hiyo ni tofauti na vita nyinyingine za mitandaoni kama iliyowahi kumuhusisha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

Jana alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kuelezea kuwa watu ambao wamepanga njama za kumuua.

Waziri Kigwangalla aliandika kuwa tangu awe waziri maisha yake yamekuwa hatarini mpaka kufikia hatua ya kuwekewa ulinzi na Serikali.

Advertisement

Amesema hatarajii kufanya mkutano na waandishi wa habari baada ya kushauriwa na watu wengi, lakini timu yake “imefanya kazi nzuri” kwa kumpa uthibitisho wa majina ya maadui zake.

“Bahati mbaya hakuna cha kunichafua nacho. Wanapika hadithi za kitoto na kurudia tu. Walidhani ningekaidi maelekezo ya Mhe Rais juu ya mgogoro wa ndani ya wizara yetu ili Rais achukie aniondoe, wakakwama,” ameandika Waziri Kigwangalla.

“Wakaona wafanye mwendelezo kupitia gazeti, sijataka kujibishana nalo, tutakutana mahakamani ambapo mbivu na mbichi zitajulikana, ukweli utawekwa wazi na rekodi itakaa sawa. Sijashangaa kuwa wahusika ni wale wale wa kipindi kilichopita.”

Ameeleza kuwa sababu ya sakata hilo ni maslahi binafsi ambayo hayatekelezeki bila ridhaa ya waziri, na bahati mbaya yeye ndio Waziri.

Kigwangalla alisema walitamani asiwepo ili watafune pesa za Serikali, lakini wamekwama na kwamba ataendelea kudhibiti kimya kimya.

“Kwa wanaokumbuka wakati nimelazwa ICU na baadaye wodini, ilikuwa ngumu sana kunitembelea na kuniona. Paliwekwa ulinzi mkali sana na watu wote walizuiliwa kuingia isipokuwa kwa kibali cha Ikulu, hadi mawaziri wenzangu hawakuruhusiwa,” amebainisha waziri huyo.

“Nilishangaa sana lakini niliambiwa ndiyo hivyo. Baadaye nikaja kujua kuwa kuna watu walipanga njama za kuniua na hiyo ingeweza kuwa fursa kwao kunimalizia. Baada ya kuteuliwa tu wizara hii kulizuka mtafaruku mkubwa sana juu ya usalama wangu. Nilifuatiliwa kila kona mpaka Serikali ikanipa walinzi, nilibisha kwa kuwa sipendi attention sana lakini nililazimishwa na kuambiwa nipo kwenye threat (tishio)! Sikuwa na option.”

Ameeleza kuwa alianza kuishi kwa hofu na mashaka, hivyo baada ya ajali alilazimika kuwa makini zaidi na kwamba hata imani yake kwa kila mtu ilipungua. “Novemba 2019 nililetewa taarifa za kutisha, nikaongeza umakini. Team yangu imenisihi nisiweke majina hadharani na kwamba wanawafuatilia wahusika kwa ukaribu na watazijulisha mamlaka kwa hatua stahiki zaidi,” amesema.

“Watu wa karibu sana na mimi nimewapa mpango na taarifa zote na wanajua cha kufanya endapo chochote kitanitokea. Kuna mbinu nyingi za mapambano. Tuendelee tu! #HK”

Kutokana na andika hilo, wafuasi wa akaunti hiyo wamempa pole na kumtaka kuwa makini lakini aendelee kupambana.

Kabla ya andiko hilo, Waziri Kigwangalla alionyesha kuwa na msuguano na wafanyakazi wa moja ya magazeti.

“Kuna jamaa wa gazeti fulani wanaotumiwa na watesi wangu, waliwahi kumuandama waziri fulani wa maliasili na utalii huko siku za nyuma mpaka akawapa hela ndiyo wakaacha, wakaanza kumsifia. Mimi siyo mtu wa aina hiyo! #HK” ameandika.

Pia juzi aliandika yeye ni mtemi mwenye asili ya vita kushinda, hivyo hupigana bila kujali nani atadhurika.

“Aliyenitia kidole jichoni sasa akae sawa. Naanza kujibu mashambulizi. Aliyetaka vita sasa ameipata! Sijawahi kuwa dhaifu wala mnyonge. Sijawahi kukubali kuonewa, kukandamizwa wala kunyanyaswa maishani mwangu. Asonijua basi afuatilie historia yangu. Twende kazi,” ameandika.

Mwananchi ilipotaka uhakika kama ni yeye aliyeandika kilichopo kwenye akaunti hiyo, Kigwangalla alijibu: “Sijamjibu mtu, nimeactivate (nimeamsha) fight mode (hali ya mapambano). Huu ni 2020, ni mwaka wa mapambano.”

Katikia ujumbe mwingine ameandika kuwa wanaomfuatilia wamefanikiwa kumfikisha katika ukomo wa uvumilivu wake.

“Kuna wakati nilikata tamaa nikataka kujiuzuru uongozi wa umma, lakini nikaja kufikiri upya, ‘hivi ni nani atafanya kazi hizi?’ Kama watu wema wanaopigwa fitina na majungu wakisusa na kuacha kazi za umma za kujenga nchi, ni nani atakayefanya?” ameandika.

“Ukiwa waziri wa maliasili na utalii ukakuza idadi ya watalii kwa kasi, ukaongeza mchango wa sekta yako kwenye pato la Taifa, ukadhibiti ujangili, ukazuia ubadhirifu/rushwa/matumizi mabaya ya ofisi/uzembe, badala ya kupendwa na kuungwa mkono watu wanakushambulia. Ukijiuzuru unakuwa umewapa raha na ruhusa ya kuendelea na mambo yao.”

“Kwa kuwa wao na washirika wao wamenifikisha ukomo wa uvumilivu wangu, nimewapeleka mahakamani, mahakama itaamua. Washirika wao wamewadanganya kwa rushwa, sasa wakawape ushahidi huko mahakamani, nitawafilisi kuanzia kampuni hadi wao binafsi.”

Alisema hata alipopata ajali kuna mtu alisema “bora angekufa” na kwamba ameshamjua na amsamehe.

Amesema kuna watu wawili walipanga mbinu za kumdhuru, pengine kumuua, lakini Mungu akamlinda na kwamba hawataweza kumuangusha.

“Naingia vitani kwa silaha zote. Usiombe kunifikisha hapa. Twende kazi sasa,” amesema.

Ugomvi na Katibu Mkuu

Hivi karibuni Rais John Magufuli alilazimika kumpa siku tano Kigwangalla na katibu wake mkuu, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo angetengua uteuzi wao.

Rais Magufuli alielezea kusikitishwa na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya wawili hao, hali inayosababisha shughuli za wizara kusuasua.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa,” alisema Rais.

“Siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana. Kuna mambo mengi hayaendi, katibu mkuu hamheshimu waziri na waziri naye hataki kwenda na katibu mkuu, siwezi kuvumilia hilo.”

Muda mfupi baada ya Rais Magufuli kutoa agizo hilo, Kigwangalla aliandika Twitter akisema: “Kazi ya urais ni ngumu sana. Tulioteuliwa na Mhe Rais kumsaidia utendaji/usimamizi wa maeneo mbalimbali hatupaswi kumuongezea Rais frustrations nyingine zaidi. Sisi kwenye wizara yetu, bada ya kikao na Chief Secretary tulimaliza tofauti zetu na sasa hali ni shwari.”

Angepiga risasi

Lakini kauli tata ni mambo yanayojitokeza mara kwa mara katika akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Septemba mwaka jana, aliandika ujumbe unaopingana na kanuni za utawala wa sheria za kukamata watuhumiwa na kuwapeleka mbele ya vyombo vya haki waadhibiwe.

“|Kama ningekutana na mmoja wa majangili waliokamatwa Septemba 3, ningempiga risasi na kumuua,” aliandika wakati akieleza jinsi wizara yake kwa kushirikiana na vikosi mbalimbali vya kuzuia ujangili walivyokamata vipande 338 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh4.40 bilioni.

“Mtu ana jeuri ya kuwinda twiga, mnyama ambaye ni nembo ya Taifa katika zama hizi za (Rais John) Magufuli? Mtu wa aina hii akinikuta porini namuua na yeye hapo hapo. Si jambo la mzaha ni dharau kupindukia,” alisema.

Kauli hiyo ilizua mjadala, huku wachangiaji wakisema kauli kama hizo zinaweza kutumiwa na wananchi wenye nia ovu kudhuhuru maadui zao na kusingiuzia kuwa ni majangili.

Malumbano na January Makamba

Julai mwaka jana, Waziri Kigwangalla aliingia katika malumbano na Makamba kuhusu mradi wa kupandisha watalii Mlima Kilimanjaro kwa kutumia viberenge.

Malumbano hayo yaliiibuka baada ya akaunti ya Twitter ya Haki Ngowi kuweka taarifa kuwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inatarajia kuanzisha usafiri wa kutumia magari ya umeme yanayotumia nyaya za juu kupeleka watalii mlima huo.

Baada ya andiko hilo, Makamba alichangia suala hilo kwa kusema: “Itabidi watu wetu wa mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza kabla hawajaanza na tutafanya tathmini ili kujua matokeo kwa mazingira na mkakati wa kudhibiti.”

Lakini Kigwangalla akamjibu: “Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake? Hizi haziharibu mazingira. Cable car inapita juu inaharibu mazingira gani?

“Zaidi ya ekari 350,000 za misitu zinapotea kila mwaka nchini. Ipi risk (janga) kubwa? Watu wa mazingira wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano.”

Pia siku iliyofuata aliandika: “It’s a beautiful Monday (Ni Jumatatu nyingine nzuri) tunaanza upya. Mtani wangu (Makamba) anajua wazi kuwa kila mradi tunaoufanya lazima ufanyiwe EIA (Tathmini ya athari ya mazingira).”

Baadaye Makamba aliomba jambo hilo liishe kwa kuwa wanajenga nyumba moja, ya Watanzania.

Kauli za viongozi

Kauli zake hazijapokelewa vizuri na wadau. mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema kauli yake kuwa kuna watu wanataka kumuua si ya kupuuzwa, “ukizingatia kuwa yeye ni waziri katika Serikali. Natarajia kuona Jeshi la Polisi likuchukua kwa uzito mkubwa kauli hii”.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema si kitu cha kawaida kwa waziri anayefahamu taratibu kulalamikia usalama wake mitandaoni.

“Nimeona nimeshangaa maana kwa nafasi yake anafahamu taratibu za nchi ikitokea mtu usalama wake upo hatarini, afuate hatua gani na aende wapi kuripoti. Yeye ana uwezo wa kuifikia mamlaka yake ya uteuzi tofauti na ilivyo kwa mwananchi wa kawaida,” alisema.

“Sasa kama waziri analalamikia usalama wake hadharani namna hii kwa watu wa kawaida, hali inaweza kuwa ya hatari zaidi ingawa hiyo haimaanishi kuwa waziri hatakiwi kuwa salama. Jambo la muhimu afuate taratibu aripoti kama hazifahmu awatumie wanasheria wa wizara.”

Mwanachi aliyejitambusha kwa jina la V Lupia, amemshauri Kingwangalla aende mahakamani au kuwashitaki polisi kwa kuwa inaonekana anawajua watesi wake.

“Lowasa alijisemea shida ni uwaziri mkuu. Je na yeye shida ni uwaziri?” alihoji.

Mwananchi mwingine, Nyaonge James, alisema huwa na wasiwasi anapoona viongozi walioaminiwa na rais wa nchi wanapokwenda kwenye mitandao ya kijamii kuandika maneno yanayolenga mtu fulani au vitu fulani.

“Kwa nini wasimalizane huko maofisini kwao. Utafikiri hawana skills za uongozi?” aliandika.

Advertisement