WhatsApp lawamani kuruhusu kuingilia mawasiliano

Programu mpya iliyotolewa ambayo inaweza kutumia udhaifu uliopo katika mtandao wa WhatsApp unaomilikiwa na kampuni ya Facebook inakuruhusu mtu kuweka maneno kwenye maandishi ambayo mhusika hakuyaandika.

Timu ya wataalamu wa kampuni ya usalama wa mtandao Checkpoint imeonyesha jinsi programu hiyo inavyoweza kutumiwa kumegua maneno kwenye ujumbe ndani ya nukuu za jumbe, na hivyo kufanya ionekane kana kwamba mtu alisema kitu ambacho hakukisema.

Mtafiti Oded Vanunu ameiambia BBC kuwa programu hiyo imewawezesha “watu wenye nia mbaya “ kubadili mawasiliano kwenye mtandao huo.

Hadi sasa Facebook haijatoa kauli yoyote kuhusiana na shutuma hizo.

“Unaweza kubadili kabisa kitu ambacho mtu anakisema ,”Alisema Bwana Vanunu.” Unaweza kuharibu kabisa maneno ya nukuu ya mtu aliyoisema,” alisema Vanunu.

Programu hiyo pia humruhusu mshambuliaji kubadili jinsi mtumaji wa ujumbe anavyotambulika, na hivyo kuwezesha kubadilishwa kwa chanzo cha ujumbe na kuonekana kama ulitumwa na chanzo kingine tofauti.