Zanzibar yafanya uchaguzi wa kwanza wa Rais mwaka 1980

Tangu yalipofanyika Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964, iliwachukua Wazanzibari zaidi ya miaka 16 kuanza kutumia haki yao ya kupiga kura kumchagua rais wao.

Mbali na kushiriki uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kati ya mwaka 1964 na 1980 Zanzibar haukuwahi kufanyika uchaguzi wowote wa rais wa visiwa hivyo.

Uchaguzi wa kwanza Zanzibar ulikuwa Julai 1957 na ulihusisha nafasi za wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Vyama vilivyoshiriki ni Afro-Shirazi (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP).

Katika uchaguzi huo, ASP ilishinda viti vitano kati ya sita vilivyogombewa.

Baada ya uchaguzi huo, kuna uchaguzi uliofanyika Januari 17, 1961, Juni Mosi, 1961 na Julai 8 hadi 11, 1963.

Kwa mujibu wa kitabu cha Elections in Africa: A Data Handbook (ukurasa 872), baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Karume alitangaza kuwa “hakutakuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 60 ijayo”.

Katika ukurasa wa 10576 wa jarida Congressional Record: Proceedings and Debates of the ..., Volume 115, Part 8, la Aprili 28, 1969, Sheikh Abeid Karume amekaririwa akisema: “...Hakuna uchaguzi utafanyika Zanzibar kwa angalau miaka 60 ijayo. Uchaguzi ni chombo cha mabeberu cha kuwakandamiza wananchi.”

Maneno hayo yamekaririwa pia na kitabu cha Tanzania: The Story of Julius Nyerere Through the Pages of Drum cha waandishi Mohamed Amin, Annie Smyth na‎Adam Seftel.

Mwandishi William Edgett Smith katika ukurasa wa 181 wa kitabu chake cha mwaka 1971 cha We Must Run While They Walk: A Portrait of Africa’s Julius Nyerere, ameandika kuwa Karume alitamka maneno hayo mwaka 1968 alipohojiwa na gazeti la Tanzania, The Standard’ (sasa Daily News).

Mchakato wa kumpata Rais wa Zanzibar kwa njia ya kupigiwa kura ulianza Jumamosi Septemba 6, 1980 wakati Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya CCM iliyokuwa inasimamia shughuli zote za Serikali ya Zanzibar ilipokutana mjini Dar es Salaam, kupendekeza majina ya watu wanaofaa kugombea urais.

Baada ya uteuzi wa majina ya wagombea hao, Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo ilikutana Septemba 12 na 13, ilifanya uteuzi wa mwisho wa wagombea pekee wa kiti cha Rais wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa kifungu cha 63(3) cha katiba ya CCM ya mwaka 1977, wakati uchaguzi unapowadia, Kamati Maalumu ya Kamati Kuu yenye jukumu la kuangalia na kusimamia shughuli zote za Serikali kwa upande wa Zanzibar, hufanya uteuzi wa mwanzo wa majina ya watu wanaofaa kugombea urais.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, wakati wa kuchagua kiongozi wa Serikali ya Zanzibar unapowadia, Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya CCM iliyoundwa kwa ajili ya kuangalia na kusimamia shughuli zote za Serikali ya Zanzibar itakutana na kupendekeza majina ya watu wasiopungua wawili kutoka Zanzibar ambao wametimiza umri wa miaka 30 na wanaofaa kuwa watu pekee wa kusimama katika uchaguzi wa nafasi hiyo.

Hivyo, Septemba 12, Halmashauri Kuu ya Taifa ilimteua Aboud Jumbe kuwa mgombea pekee wa urais wa Zanzibar.

Jumbe alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, makamu mwenyekiti wa CCM na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati kikao hicho kilipotaka kuanza kujadili jina la Jumbe, mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alimuomba Jumbe kuondoka mkutanoni.

Jumbe, aliyekuwa na umri wa miaka 60, alianza kuiongoza Zanzibar tangu Aprili 1972 baada ya kifo cha Abeid Amani Karume.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Zanzibar kuchaguliwa kwa kura tangu Mapinduzi ya 1964 na mara ya kwanza tangu Zanzibar ilipopata katiba yake mwaka 1979. Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili Oktoba 26, 1980.

Matokeo ya Uchaguzi huo yalitangazwa siku mbili baadaye na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar, Idris Abdul Wakili.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Abubakar Khamisi alisema sherehe za kuapishwa zingefanyika viwanja vya jengo la Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.

Hivyo, Oktoba 29, Jumbe alitangazwa rasmi kuwa rais wa Zanzibar baada ya kupata kura 174,672 za ndiyo kati ya kura 186,517 zilizopigwa katika uchaguzi huo, sawa na asilimia 93.65 ya kura zote, wakati kura za hapana zilikuwa 5,508 huku kura 6,337 zikiharibika. Jumla ya watu 199,946 walijiandikisha kupiga kura.

“Kwa hiyo kufuatana na kifungu cha 57(3) cha Sheria Namba 3 ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1980, natangaza kuwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amekuwa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,” alisema Abdul Wakil.

Kwa mujibu wa Katiba mpya ya Zanzibar, Rais anachaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Katiba ya Zanzibar ambayo ilifuta Sheria namba 5 ya mwaka 1964 ilitoa nafasi ya kuwapo kwa Baraza la Mapinduzi lenye wajumbe 35 ambalo ni chombo cha ushauri kwa Rais na Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe 125 ambalo ni sawa na Bunge.

Oktoba 30, saa 4:05 asubuhi, Jumbe alikula kiapo cha kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mbele ya Jaji Augustine Ramadhani, Jumbe alitamka: “Mimi Aboud Jumbe Mwinyi, naahidi kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwa nitaitumikia Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uaminifu.”

Saa moja baada ya kuapishwa, aliteua na kuwaapisha wajumbe 31, wakiwamo wanawake wawili, wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.

Katibu wa baraza hilo, Ali Salim alisema Jumbe aliwateua wajumbe 31 na wengine watatu waliobakia angewateua baadaye. Baraza jipya lilikuwa na wajumbe wapya 19 na 12 wa zamani. Watu wengine waliokuwa wajumbe katika baraza hilo tangu mapinduzi ya mwaka 1964 waliachwa nje.

Miongoni mwa sura mpya zilizoibuka katika baraza hilo ni za kina Abdallah Rashid, Abdallah Said Haji, Aboud Talib, Ali Mohammed Shoka, Hamid Vuai Makungu, Hamid Ussi, Hasnu Makame, Issa Mohamed Suleiman, Khamis Juma Seif, Masoud Omari, Rajabu Bakari Juma, Soud Yusuf Mgeni, Simai Mmanga Khamis, Suleiman Othman, Taimur Salehe, Ussi Khamis na Wazir Mbwana Ali.

Wanawake ambao ilikuwa mara ya kwanza kuteuliwa kuwa wajumbe wa Baraza walikuwa ni Mastura Ali Salim na Theresia Aban Ali.

Wajumbe wa zamani ambao waliingia katika baraza jipya ni Abdallah Said Natepe, Edington Kisasi, Hafidh Suleiman, Hamid Ameir, Hassan Nassoro Moyo, Idi Pandu Hassan, Khamis Darwesh, Khamis Hemed, Ramadhani Haji Faki, Saidi Idi Vuai, Seif Bakari na Yusuf Himid.

Jumapili Novemba 9, Jumbe aliteua na kuapisha Baraza la Mawaziri la serikali yake lililokuwa na mawaziri 15, kati ya hao, mwanamke alikuwa mmoja tu.

Mawaziri wote, isipokuwa watatu waliokuwamo katika Baraza la Mawaziri lililopita, hawakuwamo katika baraza jipya.

Mawaziri wawili wa baraza la zamani la Serikali ya Muungano wa Tanzania ambao ni Nassoro Moyo na Hasnu Makame walitajwa kuwa mawaziri wa Serikali ya Zanzibar.

Naibu wa zamani wa Wizara ya Elimu, Idarus Mwinyiweza alibaki katika wizara hiyo wakati naibu wa zamani wa Wizara ya Afya, Ali Mohamed Shoka aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni na Michezo. Mohamed Faki ambaye awali alikuwa Waziri wa Viwanda sasa aliteuliwa kuwa katibu wa Baraza la Mapinduzi.

Baraza jipya la mawaziri liliwajumuisha Rais; Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ramadhani Haji Faki; Waziri wa Nchi (Mipango), Ussi Hamis Haji; Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Aboud Talib Aboud; Waziri wa Fedha, Taimur Saleh Juma; Waziri wa Kilimo, Hassan Nassoro Moyo; Waziri wa Maliasili na Utalii, Simai Mmanga Hamisi na Waziri wa Viwanda, Iddi Pandu Hassan. Wengine ni Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Hamis Juma Seif; Waziri wa Elimu, Masoud Omar Said; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Hasnu Makame; Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Yusuf Soud Mgeni; Waziri wa Ardhi, Ujenzi na Nyumba, Edington Kisasi; Waziri wa Habari, Utangazaji na Televisheni, Issa Mohamed Suleiman na Waziri wa Michezo na Utamaduni, Bibi Mastura Ali Salim.

Naibu mawaziri walikuwa Usi Hamis Juma (Kilimo), Abdallah Rashid Abdallah (Mifugo), Idarus Mwinyiwesa (Elimu), Ali Mohammed Shoka (Afya) na Ali Mwinyigogo (Utamaduni na Michezo).