Zitto Kabwe sasa awekwa mtu kati

Dar es Salaam. Sasa ni wazi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amewekwa katika hali ngumu kutokana na kutuhumiwa na kunyooshewa kidole katika masuala matatu, licha ya kuyatolea majibu kwa nyakati tofauti.

Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imezua maswali kuhusu mustakabali wa kisiasa wa kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo.

Katika siku za karibuni ameingia katika malumbano na Bunge, wanasiasa wenzake ambao awali walikuwa watu wake wa karibu, na Takukuru -- kwa mujibu wa taarifa yake -- ikihitaji kumuhoji.

Pia tuhuma za kupata mgao wa fedha zilizochotwa kutoka Akaunti ya Escrow ambazo ziliwahi kuibuka bungeni, zimefufuliwa.

Miongoni mwa wanaokabiliana na Zitto ni Profesa Kitila Mkumbo ,katibu mkuu wa Wizara ya Maji, ambaye anapambana naye katika mitandao ya kijamii kuhusu ukosoaji dhidi ya kitendo cha Serikali kukopa fedha kwa ajili ya kuzitumia katika miradi ya maendeleo, wakati ikisema inatumia fedha za ndani.

Hata jimboni kwake pia amekuwa akipata misukosuko, na hivi karibuni alizuiwa kufanya mikutano na kibaya zaidi madiwani watano ndani ya jimbo lake wamekihama chama chake na kujiunga na CCM.

Zitto, ambaye kwa sasa yupo nchini Marekani, alianza kushukiwa na wabunge katika mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma kwa kitendo chake cha kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB) akitaka isiidhinishe mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa Tanzania kwa ajili ya sekta ya elimu.

Jambo hilo lililaaniwa na wabunge wa CCM, huku Spika Job Ndugai akisema watamsubiri arejee nchini ili wamuulize sababu za kufanya hivyo, na hapohapo akamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia kama kuna uwezekano wa kuwemo jinai katika kitendo hicho.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Zitto ameibua madai ya mtu mmoja ambaye zamani alikuwa mbunge na sasa ni katibu tawala, kuwasilisha malalamiko Takukuru akimtuhumu kuhusika na utakatishaji wa dola 2 milioni za Marekani (sawa na takriban Sh3.4 bilioni).

“Wala wasidhani kuwa nitaogopa kurudi Tanzania. Nitarudi mchana kweupe,” ameandika mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Vijijini.

“Nitakuwa mahakamani kusikiliza hukumu ndogo ya kesi yangu ya uchochezi na pia kesi yangu dhidi ya Rais (John) Magufuli kuvunja Katiba ya nchi...”

Licha ya kutomtaja mhusika, Mwananchi inafahamu kuwa anayelengwa ni David Kafulila, katibu tawala wa Wilaya ya Songwe, ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (NCCR-Mageuzi) kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.

“Nimesoma alichoandika Zitto. Mimi kama mtumishi wa umma sioni sababu ya kueleza chochote kwa kuzingatia suala hilo linafanyiwa kazi na vyombo vyenye mamlaka ya kuchunguza,” alisema Kafulila ambaye amerejea CCM.

“Hivyo wao Takukuru ndio wenye mamlaka ya kusema lolote kuhusu jambo wanalofanyia uchunguzi.”

Pamoja na majibu hayo ya Kafulila, Mwananchi inafahamu kuwa mwaka 2017, katibu tawala huyo aliandikia barua kwa Takukuru, Taasisi ya Kuchunguza Makosa ya Jinai Uingereza (SFO), Spika na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kutaka kuchunguzwa kwa ukweli wa baruapepe zilizovuja kuonyesha mchakato wa malipo wa fedha hizo kutoka benki ya Standard Chartered ya Uingereza kwenda kwa Zitto.

Wakati huo, Takukuru ilimhoji na Zitto amethibitisha suala hilo, akidai kuwa chombo hicho kilimtajia aliyewapa taarifa hizo.

“Nilipoulizwa na Takukuru, nani kawaeleza upuuzi huo wakasema wameletewa barua na mbunge mmoja wa zamani (hivi sasa katibu tawala),” alidai Zito.

“Nikawaambia mbunge huyo kawadanganya na mlipaswa kujiridhisha kwanza kwa kuwa Standard Chartered ni benki kubwa na haiwezi kujiingiza katika upuuzi.”

Lakini mkurugenzi mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alikanusha kuwepo kwa madai hayo.

“Sijui kuhusu suala hilo, hakuna hilo jambo,” alisema alipoulizwa kuhusu Zitto kuchunguzwa kwa utakatishaji fedha.

Madai ya usaliti

Kabla ya Zitto kupambana na Kafulila, Spika Ndugai alielezea uwezekano wa Bunge kumshughulikia mwanasiasa huyo, akirejea sakata la Bunge la Marekani kutaka kumwondoa rais wa nchi hiyo, Donald Trump kwa vitendo vya kukosa uzalendo.

Spika Ndugai alisema hayo wakati akihitimisha hoja iliyowasilishwa na mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel aliyetaka wabunge wamuunge mkono kufikia uamuzi wa kumchukulia hatua Zitto kutokana na kuiandikia barua Benki ya Dunia ili izuie mkopo kwa Tanzania.

Ndugai aliwaambia wabunge kuwa jimboni kwake baadhi ya shule wanafunzi hawana madawati, wanakalia vigoda vya miguu mitatu na hivyo kitendo cha Zitto ni usaliti kwa kuwa fedha hizo zingesaidia kuokoa changamoto za elimu na kubainisha kuwa Zitto akirejea nchini watamuuliza alikuwa akilenga nini.

Katika majibu yake kwa Bunge na Ndugai, Zitto alisema hakuna tofauti ya kisera katika suala la watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.

“Ilani ya CCM iliahidi hilo wananchi mwaka 2015, vyama vya upinzani viliahidi hilo na mbili ya tatu wanaunga mkono hilo. Hata ilani ya CCM mwaka 2015 walitaka watoto waliopata ujauzito warudi shuleni,” ameandika.

Moja ya sababu za benki hiyo kuzuia mkopo huo ni suala la watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni, kuzuiwa kuendelea na masomo, ikitaka Serikali ionyeshe mpango utakaoonyesha wanapata haki hiyo.

Zitto pia anapambana na Profesa Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo. Kwa mara nyingine, profesa huyo alimkosoa Zito kwa kuendesha kampeni ya kuzuiwa mkopo huo.

Kitila alidai Benki ya Dunia walimtumia Zitto kuzuia mkopo, lakini walikuwa na sababu nyingine.

Alisema anamshangaa Zitto kwa jitihada hizo wakati alikuwa anapinga taasisi za fedha za kimataifa kutoa mikopo na misaada yenye masharti.

Zitto na Kitila

Profesa Mkumbo pia alijibizana na Zitto kuhusu fedha za ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ikiwa zimepita takribani siku tatu tangu Serikali isaini mkopo wa Sh3.3 trilioni kwa ajili ya awamu ya pili kutoka Morogoro, Makutupora hadi Singida.

Mkopo huo uliratibiwa na benki ya Standard Charterd na unajumuisha wakopeshaji 17 ikiwamo Serikali ya Denmark na Sweden.

Wakati Zitto akihoji fedha zinazotumika katika ujenzi wa mradi huo, Profesa Mkumbo alisema hoja ya msingi ni hizo fedha zinakwenda wapi.

“Tunajua kwa dhati fedha inayokopwa inakwenda kwenye miradi ya maendeleo na inaonekana. Ni wewe uliyeshauri kwa bidii kuwa tusijenge miradi kwa hela za ndani,” ameandika Profesa Mkumbo katika ukurasa wake wa Twitter.

Katika majibu yake kwa Kitila, Zitto anasema ni kweli mwaka 2016 alishauri kuwa hawawezi kujenga mradi mkubwa wa reli kwa kodi za wauza nyanya.

“Imewachukua miaka minne kuelewa hilo na baada ya reli kuishia Morogoro, makandarasi kutolipwa na kuahirisha uzinduzi mara saba,” ameandika.

Kwa mujibu wa Zitto, ujenzi ulianza na fedha zikatoka kwenye mzunguko nchini na matokeo hali ya maisha ya wananchi ikawa mbaya.

“Mimi sijasema lolote, nimemwaga data tu kutoka Benki Kuu kuhusu Deni la Taifa. Kwamba wakati uchumi unakua kwa asilimia nne mpaka tano kwa mwaka, deni la nje linakua kwa zaidi ya asilimia 18 kwa mwaka,” alisema.

Profesa Mkumbo alifafanua alichokuwa akimaanisha katika ujumbe wake kwamba fedha ambazo Serikali inakopa ni kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Alisema katika kipindi alichoingia wizara hiyo wameshakopa Sh1 trilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika miji 28, Sh500 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji mkoani Arusha na Sh600 bilioni kwa jili ya mradi mkoani Tabora.