Zitto aeleza ACT itakavyoendesha nchi ikishinda uchaguzi mkuu

Kutoka kushoto viongozi wakuu wa chama cha ACT Wazalendo,Maaalimu Sefu Sharif Hamad,Juma Duni Hajj,Zitto Kabwe na mgeni mwaalikwa Makamu wa Rais wa chama cha MDC kutoka Zimbabwe,Tendai Biti wakiiimba nyikmbo za chama wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omari Fungo

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema endapo chama hicho kitashinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kitajenga uchumi unaokua kwa asilimia 11 na utakaokuwa jumuishi.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho Dar es Salaam jana, Zitto alisema Serikali itakayoundwa na chama hicho itaimarisha pato la Mtanzania kwa wastani wa dola za Marekani 2,300 kwa mwaka.

“Tunakwenda kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hadi kufika chini ya asilimia tatu na kupunguza umaskini hadi kufikia angalau asilimia tano kutoka asilimia 28 ya sasa. ACT inakwenda kujenga Tanzania ambayo kila Mtanzania atakuwa na Hifadhi ya Jamii na hivyo bima ya afya,” alisema Zitto.

Akifafanua zaidi, Zitto alisema katika kipindi cha miaka mitano kuna Watanzania zaidi ya milioni mbili walioingia katika lindi la umaskini baada ya biashara zao kufungiwa na kushindwa kulipa mikopo.

Alisema katika kipindi hicho miradi muhimu ya kiuchumi ukiwamo wa Ukanda Maalumu kiuchumi wa Bagamoyo (EPZ), ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), chuma cha Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma na mradi wa magadi soda Engaruka ama imekwamishwa au imetekelezwa kwa gharama kubwa zaidi.

“Miradi yote hii ingekuwa ni fedha zinazoingia nchini kwenye uchumi na Serikali isingetumia kodi za wananchi. Ajira nyingi zingetengenezwa na shughuli za kifungamanisho zingeimarika na kukuza shughuli nyingi za uchumi,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema zao la korosho linalolimwa kwa wingi zaidi katika mikoa ya Lindi na Mtwara limekuwa shubiri.

“Leo wakulima wa korosho wanaishi kwa shida na taabu kubwa, wamerudi kwenye ufukara, wamefukarishwa... Hatua hiyo ilikuja baada ya Serikali kusitisha miradi kwa ajili ya mradi kiwanda cha kuchakata gesi asilia Lindi (LNG),” alisema.

Akizungumzia miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, Zitto alisema imegeuka kuwa kero kwa wananchi kwa kuwa akiba ya fedha za kigeni imekauka kwenye hazina ya Taifa na kudidimiza ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, Jumatano wiki hii, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema hadi Desemba 2019, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,567.6, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 6.4, ikiwa juu ya lengo lililokubalika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) la miezi isiyopungua 6.

Mbali na hilo, Zitto alizungumzia watumishi wa umma, akisema “tangu Serikali hii iingie madarakani, hakuna nyongeza ya mshahara, kupanda vyeo wala motisha, kisingizio kikiwa ni ‘Serikali inajenga uchumi.’

Alisema pia watumishi wamekuwa waoga kutoa ushauri wa kitaalamu katika masuala makubwa yanayohitaji taaluma zao.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, alisema katika kipindi cha miaka mitano, Watanzania wamekuwa na hofu ya maisha kutokana na kubanwa kwa demokrasia, uhuru wa kujieleza na anguko la uchumi.

“Kila kundi katika jamii limeguswa na misukosuko ya kimaisha. Iwe ni wanasiasa, wanahabari, viongozi wa dini, wanafunzi wa elimu ya juu, wanawake, vijana, wazee, wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara kila mmoja ana hofu,” alisema Zitto.

“Kila mtu amezibwa mdomo kwa kupenda au kwa hofu, wanasiasa wanapishana mahakamani, mahabusu zimejaa watuhumiwa wa kinachoitwa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, wakosoaji wanashughulikiwa kama wahalifu,” alisema.

Kwa upande wake Kiongozi wa Upinzani katika Bunge la Zimbabwe, Tendai Biti alisema wakati dunia iko katika mshtuko wa ugonjwa hatari wa corona, Bara la Afrika limekumbwa na ugonjwa wa ukandamizaji wa demokrasia.

Biti anayetokea Chama cha Movement for Democratic Change (MDC), alivilaumu vyama vya ukombozi Afrika kwa kupoteza malengo ya ukombozi na kubaki kukandamiza demorasia.

“Nimesafiri kutoka Zimbabwe, nimepitia katika viwanja viwili vya ndege na kila nilipofika nimekuta wamevaa vifunika uso, kutokana na ugonjwa wa corona,” amesema Biti.

“Lakini kuna ugonjwa ni wa kisiasa, wa kutovumilia, wa kidikteta uliojaa katika Afrika unaovuruga utu wetu,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo alisema “Tumeona watu wakikamatwa, waandishi wa habari wakikamatwa, tumeona makosa ya uchochezi yaliyokuwa yakitumiwa na wakoloni yakiwa makosa makubwa,” alisema.

Aligusia hata kesi ya viongozi wa Chadema, akisema hata wabunge wameshitakiwa na wametakiwa kulipa faini kubwa,” alisema.