Zitto afungua kesi kutetea U-CAG wa Profesa Assad

Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe amefungua kesi ya kikatiba akipinga Sheria ya Ukaguzi ya Taifa namba 11 ya mwaka 2008 inayoweka vipindi viwili vya mtu kushika wadhifa wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), amechukua hatua hiyo kwa kile alichodai kuondolewa kwa Profesa Mussa Assad katika wadhifa huo kabla ya muda wake wa utumishi kwa nafasi hiyo, kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Profesa Assad aliteuliwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na alimaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano kwa mujibu wa sheria hiyo, Novemba 5, 2019.

Sheria hiyo kifungu cha 6(1) kinaeleza kuwa mtu aliyeteuliwa kuwa CAG atashika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitano na baada ya kipindi hicho anaweza kuongezewa kipindi kingine cha miaka mitano kuhudumu katika wadhifa huo.

Profesa Assad baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano, Rais John Magufuli hakumwongezea kipindi kingine cha pili cha miaka mitano, kama sheria hiyo inavyoelekeza, badala yake alimteua Charles Kichere kushika wadhifa huo.

Hata hivyo, sheria hiyo haiweki hilo kama sharti la lazima kwani imesema tu kuwa mtu huyo atakuwa na sifa ya kuongezewa kipindi kingine, hivyo inaacha ridhaa kwa mwenye mamlaka ya uteuzi ambaye ni rais, kama akiona inafaa kumwongezea kipindi kingine.

Lakini Zitto amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), CAG wa sasa, Kichere na CAG mstaafu, Profesa Assad.

Katika kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2020, kwa mujibu wa hati ya madai na hati ya kiapo chake, Zitto anadai kuwa sheria hiyo inakiuka masharti ya Katiba Ibara ya 144(1).

Ibara hiyo inaeleza kuwa CAG ataondoka katika wadhifa huo baada ya kufikisha umri wa miaka 60, au umri mwingine wowote utakaowekwa na sheria itakayotungwa na Bunge.

Sheria ya Ukaguzi, mbali na kuweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, kifungu hicho cha 6(2) kinaweka umri wa kustaafu wadhifa wa CAG kuwa ni miaka 65.

Hivyo, Zitto katika kesi hiyo anadai kuwa kifungu hicho cha Sheria ya Ukaguzi kuweka ukomo wa vipindi viwili vya utumishi wa wadhifa wa CAG ni kinyume cha Katiba.

Vile vile, mwanasiasa huyo anadai kuwa uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Profesa Assad katika wadhifa huo kabla ya kufikisha miaka 65 ni kinyume cha kifungu cha 6(2) cha sheria hiyo na Katiba.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo chake kinachounga mkono shauri hilo, Zitto anadai kuwa kulingana na maelezo ya wasifu wake, Profesa Assad alizaliwa Oktoba 6, 1966 na hivyo Novemba 2019 alikuwa hajafikisha umri wa miaka 65 wa kustaafu.

Kwa maelezo hayo, Zitto anadai kuwa hata uteuzi wa Kichere kushika wadhifa huo ni kinyume cha Katiba, kwani uamuzi wa Rais Magufuli kumteua kushika wadhifa huo, Novemba 3, 2019, alikuwa amemwondoa Profesa Assad wakati hajafikisha umri wa miaka 65 wala 60.

Hivyo, pamoja na kupinga sheria hiyo ya Ukaguzi kuweka ukomo wa utumishi katika wadhifa huo, pia anapinga uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Profesa Assad katika wadhifa huo.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Lameck Mlacha, akishirikiana na Jaji Benhajj Masoud na Jaji Juliana Masabo.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani ambayo Mwananchi limeiona, kesi hiyo imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 28, mwaka huu.

Hati hiyo ya wito pia inamtaka Zitto kufika mahakamani siku hiyo bila kukosa na kuwasilisha mahakamani nyaraka zote ambazo anakusudia kuzitumia katika kesi hiyo.