Ndugai asema hatima ya CAG, Halima Mdee kujulikana mkutano ujao wa Bunge

Muktasari:

Bunge limemaliza vikao vyake jijini Dodoma leo Jumamosi Februari 9, 2019 huku Spika, Job Ndugai akisogeza mbele kueleza taarifa za kuhojiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee


Dodoma. Bunge limemaliza vikao vyake jijini Dodoma leo Jumamosi Februari 9, 2019 huku Spika, Job Ndugai akisogeza mbele kueleza taarifa za kuhojiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Januari 21, 2019 Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilimhoji Profesa Assad aliyeitwa mbele ya kamati hiyo kueleza kauli yake kuhusu “udhaifu wa Bunge.”

Profesa Assad aliitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.

Alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi.

Mbali na Assad, Januari 22 kamati hiyo ilimhoji Mdee ambaye aliunga mkono kauli ya CAG kuhusu Bunge.

Akizungumza bungeni leo, Ndugai amesema taarifa za kamati hiyo ziko tayari lakini muda haukutosha kuzisoma hivyo zitasomwa Bunge lijalo.

"Waheshimiwa wabunge  taarifa za kamati ya maadili ziko tayari lakini tunakosa muda kama mnavyoona wenyewe,  tutazileta katika mkutano ujao," amesema Ndugai

Amesema hana pingamizi na Bunge kukosolewa lakini si kwa kushambulia kama wanavyofanya wengine.

"Tushauriane, tusaidiane lakini tusidharauliane, haiwezekani mtu mmoja kutoka nje na kushambulia Bunge, sisi sote hapa ni watu wazima na tumechaguliwa na Watanzania," amesema.