Magufuli awaongoza mamia kumuaga Mengi Dar

Rais John Magufuli akiwasili katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Reginald Mengi. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Mwili wa aliyewahi kuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi unaagwa leo Jumanne katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
  • Mengi aliyezaliwa Mei 29, 1942 alifariki usiku wa kuamkia Mei 2  akiwa Dubai katika Falme za Kiarabu na mwili wake unatarajiwa kuziwa Alhamisi ya Mei 9 mkoani Kilimanjaro.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameungana na mamia ya waombolezaji katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Pamoja na Rais Magufuli kuhudhuria shughuli hiyo leo Jumanne Mei 7, 2019, viongozi wengine waliohudhuria pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, viongozi wastaafu, viongozi wa dini, kisiasa na watu mbalimbali.

Awali, SheIkh wa Mkoa wa Dar es Salaama, Alhad Musa Salum amewataka Watanzania kumuenzi Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia Mei 2, 2019 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu kwa vitendo kutokana na mambo mema aliyoyafanya kwenye jamii wakati wa uhai wake.

Amemtaja Mengi kama muasisi wa kamati za amani za mikoa na siku zote alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha amani, upendo na utulivu vinaendelea kutawala.

Kwa upande wake, Askofu Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Nelson Kisare amewataka viongozi kutumia  nafasi walizonazo  kubadili maisha ya Watanzania kwa kutumia rasilimali zilizopo Tanzania.