MAUAJI YA MWANAFUNZI SCOLASTICA: Yaliyojitokeza mwanzo hadi mwisho kesi ya mauaji ya mwanafunzi Humphrey

Kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya sekondari Scolastica, Humphrey Makundi (16), ilifikia tamati Juni 3, 2019 kwa mshitakiwa mmoja kuhukumiwa kunyongwa na wawili kifungo cha miaka minne jela kila mmoja.

Katika kesi hiyo kuna mambo saba muhimu yaliyotawala usikilizwaji wa shauri hilo lililokuwa likivuta hisia za watu wengi ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro, kiasi cha kufanya chumba cha mahakama kuwa hakitoshi.

Katika kesi hiyo, Jaji Firmin Matogolo alimhukumu mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha adhabu ya kifo, wakati mmiliki wa shule, Edward Shayo na mwalim Laban Nabiswa wakienda jela miaka minne kila mmoja.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha pili, aliuawa usiku wa Novemba 6, 2017 kwa kushambuliwa kwa panga na mlinzi, na maiti yake kupatikana mto Ghona uliopo takribani mita 300 kutoka shuleni.

Hata hivyo, mwili huo ulipoopolewa Novemba 10, 2017 haukutambuliwa na kusababisha uzikwe na Manispaa ya Moshi siku mbili baadae, lakini ukafukuliwa kwa amri ya mahakama Novemba 17, 2017.

Washtakiwa walifikishwa kortini kwa mara ya kwanza Novemba 27, 2017 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi lakini kesi ilianza kusikilizwa rasmi Aprili 2, 2019 mbele ya Jaji Matogolo.

Waandishi kuzuiwa kurekodi

Siku ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi hiyo, waandishi wa habari walijikuta katika wakati mgumu pale Jaji Matogolo alipozuia kurekodi ushahidi, isipokuwa yeye, mawakili na wazee wa mahakama.

Badala yake, Jaji Matogolo aliwataka waandishi kusikiliza tu kama watu wengine, jambo ambalo liliibua sintofahamu hadi wanahabari walipokutana na uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.

Siku hiyo, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Dk Alex Mremi alikuwa akitoa ushahidi wake kuhusiana na uchunguzi wa kisayansi wa mwili wa marehemu ili kubaini sababu za kifo.

Baada ya wanahabari kukutana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Frank Mahimbali na yeye kuwasiliana na Jaji Matogolo, waliruhusiwa kuendelea na majukumu yao ya kurekodi kesi hiyo.

Ilielezwa kuwa uamuzi wa Jaji ulitokana na kutokuwa na uhakika kama wote wanaorekodi ni wanahabari, hivyo kukawa na mashaka ya upotoshaji, lakini alihakikishiwa wote ni wanahabari.

Wapigapicha kubughudhiwa

Wapigapicha za magazeti na vituo vya Runinga, nao walijikuta katika wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yao, kwa kupata vikwanzo kutoka kwa baadhi ya ndugu wa washitakiwa.

Mbali na ndugu hao, Wakili Elikunda Kipoko ambaye alikuwa akimtetea mshitakiwa wa pili, Edward Shayo, naye alikuwa akizuia mawakili kupigwa picha bila kupata ridhaa yao.

Baadhi ya ndugu hao wa washitakiwa walifikia kutoa maneno ya kejeli kuwa “hazijawatosha tu hizo picha kila siku mnapiga” na “tuone kama mtakula hizo picha”, kila walipowaona wanahabari.

Hata hivyo, kabla ya kutekeleza wajibu huo, wanahabari walikuwa tayari wamepewa kibali na uongozi wa mahakama wa kuchukua picha za matukio isipokuwa tu zichukuliwe kabla ya mahakama kuanza.

Kesi ndogo ndani ya kesi kubwa

Aprili 10, 2019, kuliibuka malumbano makali ya kisheria wakati upande wa mashitaka ulipotaka kutoa maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa kwanza (Chacha) kupitia kwa shahidi wa 14, Irene Mushi. Jopo la mawakili wa utetezi lililokuwa likiundwa na mawakili Elikunda Kipoko, David Shillatu, Gwakisa Sambo na Patrick Paul, walipinga vikali wakidai hayakutolewa kwa hiyari na mshitakiwa.

Wakili Shillatu aliyemtetea mshitakiwa, alisema uchukuaji wa maelezo hayo ulikiuka mwongozo wa Jaji mkuu wa Tanzania uliomo katika kijitabu chake cha muongozo kwa walinzi wa amani.

Pia, Wakili Shillatu alieleza kuwa mteja wake alifanyiwa mateso makali ili kutoa maelezo hayo ya kukiri kosa la mauaji, hivyo yasipokelewe na mahakama kama kielelezo na badala yake yakataliwe.

Jaji Matogolo baada ya kusikiliza hoja hizo aliamua kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria katika uchukuaji wake isipokuwa itafanyika kesi ndani ya kesi kuona kama mshitakiwa aliteswa.

Kesi ndani ya kesi ikasikilizwa ambapo mshitakiwa Chacha alidai kufanyiwa aina nane za mateso ikiwamo kupigwa shoti ya umeme na kuingiziwa chupa ya bia sehemu za haja kubwa.

Mateso mengine ni kuingiziwa sindano kwenye uume, kunyimwa chakula, kulazwa chumba chenye maji, kuchomwa na pasi ya umeme na kuchapwa makofi na fimbo na watu aliodai ni polisi.

Mashahidi wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo, walipinga ushahidi huo wakidai ni wa kutengeneza kwani mshitakiwa alitoa maelezo yake kwa hiyari na wala hakulazimishwa na polisi.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Jaji Matogolo alitoa uamuzi wake kuwa maelezo hayo yalichukuliwa kwa hiyari na kwamba mshitakiwa alitafuta njia tu ya kujinasua.

Maelezo ya ungamo yawa mwiba

Maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha ambayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo P8, yalionekana kuwa mwiba kwa washitakiwa kwani ndiyo yaliyowaunganisha.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa siku ya tukio alimulika tochi kuelekea eneo alilohisi kulikuwa na mtu ambaye alianza kukimbia na yeye kumkimbiza kisha kumpiga kwa ubapa wa panga. “Nilimpiga bapa mgongoni na aliendelea kukimbia, nikakimbizana naye na kuna sehemu alifika na kuanguka chini na alipasuka kwenye paji la uso. Baada ya hapo akawa katulia,” anaeleza na kuongeza;

“Nikampiga bapa la pili na ndio mauti yalipomkuta palepale. Nilimpigia simu mwalim Laban nikamwambia kuna mtu nimemkimbiza lakini sijui kama ni mwanafunzi au mtu wa nje.

“Ndipo mwalimu Laban ambaye ni Mwalimu wa nidhamu akaja. Palepale akaniuliza kama nimeshampigia mkuu wa shule, nikamjibu kuwa nilishampigia mzee wa shule mzee Shayo anakuja”.

Kwa mujibu wa Chacha, baada ya wote kukutana eneo la tukio, mshitakiwa wa pili, Shayo alikataa wazo la kumpeleka hospitali na badala yake akaagiza mwili wa mwanafunzi utupwe mtoni.

Ushahidi huo uliungwa mkono na mawasiliano ya simu ukithibitisha muda ambao Chacha anaeleza aliwaita Shayo na Nabiswa kufika eneo la tukio.

Washitakiwa wabubujikwa machozi

Mshitakiwa wa pili, Edward Shayo ndiye aliyetia fora kwa kububujikwa machozi muda wote akitoa ushahidi.

Wakati akijitetea, Shayo alieleza kuwa damu ya mtoto huyo haikuwa mikononi mwake wala mikononi mwa watoto wake na kwamba hakuwahi kumfahamu kwa jina bali aliishi nao kama watoto wake.

Mshitakiwa wa tatu, Laban Nabiswa, naye alibubujikwa machozi wakati akijitetea akisema aliteswa alipokuwa mikononi mwa polisi hadi akajikojolea na kusisitiza kuwa yeye hana hatia yoyote.

Chacha kwa upande wake, muda wote alikuwa akiina kana kwamba alikuwa hataki kuwaona mashahidi wa upande wa mashitaka hasa wale ambao ushahidi wao ulikuwa ukimgusa.

Wengi hawakuamini

Tangu kutolewa kwa hukumu ya kesi hiyo, ni kama baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki hawakutegemea na bado hawaamini kama Shayo ambaye ni mfanyabiashara tajiri amefungwa.

Hakuna anayeeleza sababu hasa kwa nini hawaamini, lakini baadhi ya jamaa wanaaamini ataachiwa huru katika hatua ya rufaa, ingawa baba wa marehemu, Jackson Makundi anasisitiza ana hatia.