Askari adai wanafunzi walikiri kusambaza picha za Magufuli akiwa amevaa Hijab

Thursday July 11 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askari polisi, Anakreti Telesphory (32) wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao ameieleza mahakama ya Wilaya ya Ilala alivyowahoji wanafunzi watatu wa Chuo Kikuu cha Kampala (Kiu) waliokiri kusambaza mtandaoni picha za Rais wa Tanzania, John Magufuli ikimuonyesha amevaa Hijab.

Wanafunzi hao ni Amenitha  Konga (19), Mariam Tweve (20) na Agnes Gabriel (21) wanaotetewa na wakili, Alphonce Nachipyangu.

Telesphory ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo aliyaeleza hayo leo Alhamisi Julai 11, 2019  mbele ya hakimu mkazi, Catherine Kihoja na wakili wa Serikali, Grace Lwila katika kesi ya jinai namba 65 ya mwaka 2016.

Akitoa ushahidi katika kesi hiyo, Telesphory alieleza kuwa majukumu yake ni kufanya doria mitandaoni na kuchambua data za kielektroniki.

Amedai kuwa Juni 13, 2016 akiwa ofisini kwake alipewa maelekezo na Inspekta Beatrice kwenda katika chuo hicho kuna mshtakiwa ametuma picha ya rais akiwa amevaa Hijab katika kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp la Human Resource Menagement.

"Tulikwenda hadi chuoni hapo tutaonana na mlezi wa mwanafunzi, Herma Frank, tukamueleza tunawahitaji wanafunzi hao na alikiri kuwa wapo akatuitia,” amesema shahidi huyo.

Advertisement

Amesema wanafunzi hao waliitwa na alifanya mahojiano na Amenitha aliyekiri kuifahamu picha hiyo na kwamba  aliituma katika kundi hilo.

Amebainisha kuwa mwanafunzi huyo alipoulizwa alikoipata, alieleza kuwa ilitumwa katika kundi la mtandao huo la Empire na rafiki yake, Mariam.

Telesphory amesema Mariam alivyohojiwa alikoitoa picha hiyo alijibu kuwa aliipata katika kundi jingine la mtandao huo la Business Administration, na kwamba ilitumwa na Agnes.

Amesema pia walimhoji Agnes aliyekiri kuitambua picha hiyo na kueleza kuwa ilitumwa katika kundi la St Mary's Ulete lakini alishindwa kukumbuka nani aliituma.

Katika maelezo yake, Telesphory amedai baada ya kufanya mahojiano hayo walijaza hati za kushikilia mali ya kila mtuhumiwa kwa ajili ya kushikilia simu zao na laini Herma kusaini kama shahidi.

Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, wakili Alphonce anayewatetea washtakiwa hao alimuhoji shahidi kama ifuatavyo.

Katika kesi hiyo washtakiwa hao watatu na mwenzao, Anene Mwansasu (23) kwa pamoja wanadaiwa Juni 9, 2016 jijini Dar es Salaam walichapisha taarifa ya uongo kupitia mfumo wa kompyuta.

Walisambaza katika mitandao ya kijamii ya WhatsApp picha hizo zikimuonyesha Rais Magufuli akiwa amevaa vazi hilo linalovaliwa na wanawake wa dini ya Kiislam, jambo ambalo si kweli.

Hakimu Kihoja ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 22 na 23, 2019 na kuutaka upande wa mashtaka kupeleka  mashahidi wa kutosha ili kesi imalizike mapema.

 

Advertisement