Uhamiaji Tanzania yachukua paspoti saba nyumbani kwa Kabendera

Erick Kabendera

Muktasari:

Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema inamhoji mwandishi wa habari za uchunguzi anayeandikia magazeti ya ndani na nje ya nchi hiyo, Erick Kabendera kuhusu uraia wake.

Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imefanya ukaguzi katika makazi ya mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera na kuchukua vitu mbalimbali ikiwamo paspoti saba za kusafiria.

Ukaguzi huo ulifanyika jana Jumatano Julai 31, 2019 nyumbani kwa Kabendera, Mbweni jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na baada ya ukaguzi huo, mwandishi huyo alirudishwa ofisi za Uhamiaji, Kurasini.

Silinde Swedy ambaye ni wakili wa Kabendera akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Julai 31, 2019 mara baada ya shughuli ya ukaguzi kumalizika alisema ukaguzi huo ulianza saa 9 alasiri na kumalizika saa 10 jioni.

Alisema katika ukaguzi huo, maofisa wa uhamiaji, “Walichukua paspoti saba za kusafiria.”

Mwananchi lilipotaka kujua hizo paspoti saba zote ni za Kabendera, wakili huyo alisema, “hapana, bali pasipoti moja ni ya kwake (Kabendera) na zingine ni za ndugu zake zilizokutwa kwake.”

Pia, Silinde  alisema wamechukua vyeti mbalimbali vya Kabendera.

Awali jana asubuhi, Kamishna wa Uraia na Paspoti wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, Gerald Kihinga akizungumza na Mwananchi alisema wanaendelea na mahojiano na mwandishi  huyo kuhusu uraia wake.

Kuhusu uraia wa ndugu zake, Kihinga alisema watakapomaliza naye mahojiano watakachobaini ndiyo kitakachowafanya kuanza uchunguzi kwa ndugu zake.

Julai 29, 2019, watu waliojitambulisha ni askari polisi waliokuwa wamevalia kiraia  walimchukua kwa nguvu nyumbani Mbweni.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania, Lazaro Mambosasa alisema waliamua kwenda kumkamata mwandishi huyo baada ya kutumiwa wito wa kufika kuhojiwa lakini akakaidi.