Baraza la Mawaziri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangazwa wiki ijayo

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi

Muktasari:

Ni serikali ya kwanza ya Rais Felix Tshisekedi

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi bado anakuna kichwa kuandaa Baraza lake la kwanza la mawaziri linalotarajiwa kutangazwa wiki ijayo.

Wananchi wa DRC watalazimika kuwa watulivu na kusubiri zaidi kabla ya kutangazwa baraza jipya la mawaziri katika utawala wa Tshisekedi, chanzo karibu na ofisi ya rais kimelieleza Shirika la Habari la Ufaransa (RFI).

Serikali mpya ya DRC iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu inatarajiwa kutangazwa kati ya Agosti 19 na Septemba 7 mwaka huu, amesema Jeannine Mabunda, Spika wa Bunge la taifa.

Kwa ombi la Rais, Felix Tshisekedi, wabunge wameitishwa kushiriki katika kikao cha Jumatatu, Agosti 19 na watajadili kuhusu kuapisha mawaziri hao wapya.

Agosti 14, Rais wa DRC alikataa kupitisha timu ya kwanza mawaziri, kwa sababu idadi ya wanawake na vijana iliyopendekezwa haikuwa inatosha.

 

Kabila kurudi mlango wa nyuma

Katika Serikali hiyo mpya ya watu 65, muungano wa FCC unaoongozwa na Rais Mstaafu, Joseph Kabila ndio utakuwa na idadi kubwa ya mawaziri, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofanyika baina ya pande mbili hivi karibuni.

Pia muungano huo wenye wabunge wengi, ndio uliotoa waziri mkuu wa DRC, Sylvestre Ilunga.

Chini ya makubaliano hayo Muungano wa CACH ulio chini ya Rais Tshisekedi utapata nafasi 23, na FCC itapata nafasi 43, akiwamo waziri mkuu.

Pamoja na wabunge 118 katika ngazi ya taifa, chama cha PPRD cha Kabila kitachukua nafasi za mawaziri 11 na manaibu mawaziri 3. Muungano wa AAB unaojumuisha vyama kadhaa vya siasa katika muungano wa FCC, utapata mawaziri watatu na naibu waziri moja. Vyama vingine vinaweza kuwa na waziri mmoja au wawili au naibu waziri, kulingana na chanzo hicho.

Makundi matatu ambayo hayana wawakilishi bungeni hayataweza kuwakilishwa katika serikali hiyo mpya.

Katika muungano wa FCC pia Kabila mwenyewe anapaswa kunufaika na kiwango cha asilimia 10 kwenye nafasi 42 zilizohifadhiwa kwa washirika wake wa kisiasa.