Mmoja afariki dunia ajali nyingine ya lori la mafuta kuteketea kwa moto nchini Tanzania

Mkuu wa Polisi wilaya ya Kahama, Annamringi Macha

Muktasari:

  • Malori mawili ya mafuta yamepinduka katika matukio mawili tofauti wilayani Kahama mkoani Shinyanga nchini Tanzania na kusababisha kifo cha utingo huku dereva akijeruhiwa

Kahama. Malori mawili ya mafuta yamepinduka katika matukio mawili tofauti wilayani Kahama mkoani Shinyanga nchini Tanzania na kusababisha kifo cha utingo huku dereva akijeruhiwa.

Ajali ya malori hayo imekuja ikiwa imepita wiki moja tangu ilipotokea ajali ya lori la mafuta ya petroli lililoanguka kisha kuwaka moto eneo Msamvu mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 94 hadi leo saa 6 mchana. Ajali hiyo ilitokea Jumamosi iliyopita Agosti 10, 2019 huku wengi waliokufa wakitajwa kukimbilia eneo la ajali kuchota mafuta yaliyokuwa yakichuruzika.

Mkuu wa Polisi wilaya ya Kahama, Annamringi Macha amesema ajali moja imetokea leo Agosti 17, 2019 katika mji mdogo wa Isaka baada ya lori la mafuta ya dizeli inayomilikiwa na kampuni ya Interpetrol ya jijini Dar es Salaam kupinduka.

“Tumechukua tahadhari kudhibiti wananchi wasisogee eneo la ajali kuapuka madhara kama yaliyotokea kule Morogoro. Nawapongeza wananchi kwa kutii amri ya kutosogelea eneo la ajali," amesema Macha.

Katika tukio la pili lililotokea Agosti 16, 2019, Kamanda Macha amesema lori linalomilikiwa na  kampuni

ya Mount Meru lilipinduka na kuteketea kwa moto.

Amesema ajali hiyo iliyosababisha kifo cha utingo ambaye jina lake halijafahamika, lilitokea eneo Shunu wilayani Kahama.

"Dereva wa lori lile alijeruhiwa na amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa matibabu," amesema Kamanda Macha

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Inspekta Dumma Mohamed amesema kikosi chake kilifanikiwa kumwokoa dereva huyo baada ya kudhibiti moto.

Lori lililopata ajali lilikuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Kigali nchini Rwanda.