Samantha wa Big Brother Africa 2014 akumbwa na tuhuma za ubaguzi Zanzibar

Muktasari:

Samantha ambaye alishiriki Big Brother Afrika mwaka 2014 pamoja na mshindi wa shindano hilo, Idris Sultan, amesambaza video akidai kubaguliwa katika hoteli moja huko Zanzibar huku Serikalui ya SMZ ikijibu tuhuma hizo.

Moshi. Raia wa Afrika Kusini, Samantha Jannsen ameibua mjadala mzito katika mitandao ya kijamii baada ya kuituhumu hoteli ya kitalii ya Vera Club Sunset Beach ya Zanzibar kwa ubaguzi wa rangi.

 Samantha aliyeshiriki Big Brother Afrika mwaka 2014 na kuwa na uhusiano na mshindi wa shindano hilo, Idris Sultan, alikuwa visiwani Zanzibar kutalii na ndipo alipokwenda katika hoteli hiyo na kuzuiwa.

 Mtalii huyo wa mara kwa mara katika visiwa hivyo katika madai yake yaliyosambaa Agosti 15,2019, alidai kusikia muziki akaamini ulikuwa ni muziki unaopigwa katika hoteli zilizopo fukwe za bahari.

 Katika madai yake aliyoyaandika ukurasa wake wa Instagram, Samantha anadai alikwenda katika hoteli hiyo akiwa na dada yake, lakini mlinzi akawazuia getini akidai hoteli ni kwa ajili ya Waitaliano tu.

 Samantha ameambatanisha mkanda wa video akibishana na mlinzi wa hoteli hiyo iliyopo Nungwi Visiwani Zanzibar, ambapo mlinzi anasikika akisema watu weusi hawaruhusiwi katika hoteli hiyo.

 “Unasema wanaruhusiwa Waitaliano tu? Hakuna mtu mweusi? Hii ni nchi ya Kiafrika. Huwezi kuja nchi ya Kiafrika halafu ukute hoteli kwa watu weupe tu. Tulishapita huko,” anasikika Samantha akihoji.

 Hata hivyo, Tume ya Utalii Zanzibar (ZCT),  imekanusha madai hayo na kueleza kusikitishwa kwake na namna tukio hilo lilivyokuzwa na vyombo vya habari vya ndani ya nchi na vile vya kimataifa.

 “Tunapenda kuwaeleza watu wote walioumizwa na maneno hayo kuwa sio sera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar na sekta ya utalii kubagua mtu kwa asili au kabila lake,” imesema.

 Katika taarifa yake ya Agosti 19,2019 iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji, Dk Abdullah J. Mohamed, ZCT imesema katika uchunguzi wake, imebaini kulikuwa na kutoelewana kati ya mlinzi na Samantha.

 “Baada ya kuwahoji uongozi wa hoteli tumefikia hitimisho kuwa kulikuwa na kupishana kwa lugha kati ya Samantha na mlinzi aliyekuwa getini kulikosababisha kutoelewana baina yao,” Imesema.

 “Mlinzi alitaka kumfahamisha Samantha kwamba sherehe ya ufukweni ilikuwa mahsusi kwa wageni wa hoteli. Ilitokea kwamba siku hiyo wageni karibu wote walikuwa kutoka Italy,” Imeeleza ZCT.

 ZCT imesema anaelewa mapokezi ya mlinzi aliyowapa akina Samantha hayakuwa sahihi na hayaendani na kanuni za ZCT ambazo zinahamasisha wageni kutembelea Zanzibar bila kujali asili yao au kabila.

 “Hatupingi uwepo wa makabila nchini lakini sio kwa namna ilivyomtokea Samantha. Hata hivyo, suala la usalama kwa sekta ya utalii ni muhimu kwa ajili ya wageni na wawekezaji,” imesema taarifa hiyo.

 Dk Mohamed amesema tayari ZCT imeshachukua hatua sahihi kuhakikisha kuwa tukio kama hilo halijitokezi tena na wataendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa sekta hiyo kutoa huduma bora.

 Pamoja na maelezo hayo, wachangiaji katika mitandao ya kijamii wameikosoa ZCT kwanza kuitetea hoteli hiyo badala yenyewe kujitokeza na pili, kuegemea utetezi wa hoteli badala ya kuchunguza.

 Katika mitandao hiyo, wachangiaji wamemtaka waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala, kuchunguza baadhi ya hoteli za kitatalii hapa Tanzania bara kuwa nazo zina chembechembe za ubaguzi.