Kampuni ya Lindi Jumbo ruksa kuchimba madini ya Graphite

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeridhia kampuni ya uchimbaji madini ya Graphite ya Lindi Jumbo kuanza ujenzi wa mitambo kwa ajili ya kuanza uzalishaji

Lindi.  Serikali ya Tanzania imeridhia kampuni ya uchimbaji madini ya Graphite ya Lindi Jumbo kuanza ujenzi wa mitambo kwa ajili ya kuanza uzalishaji.

Hayo yameelezwa jana Jumatano Agosti 20, 2019 na naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo mjini Dodoma baada ya kukutana na mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Allan Mulligan.

Mulligan alimtembelea naibu waziri huyo kwa lengo la kumtaarifu kuhusu hatua iliyofikiwa katika mchakato wa ujenzi wa mitambo, mabwawa ya maji taka na miundombinu.

Amesema Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya wananchi wake ndio maana inahimiza uzalishaji huo uanze ili kupata mapato.

Nyongo amemshukuru mkurugenzi huyo kwa kukamilisha  ulipaji wa fidia kwenye maeneo yote ya mgodi,  taratibu zinazohitajika kufuatwa kabla ya kuanza uzalishaji ikiwemo ujenzi wa bwawa la maji sumu (TFS).

“Hatupendi kuona migogoro kati ya mwekezaji na wananchi hasa katika masuala ya fidia kama ilivyotokea kwenye baadhi ya migodi, hongereni sana. Sasa nendeni mkafanye hima kukamilisha miundo mbinu na ujenzi wa plant ili muanze uzalishaji,” amesema Nyongo.

Mulligan ameeleza kuwa fidia hiyo ni Sh4.6 bilioni na ulipaji ulifanyika kwa awamu tatu, kwamba hadi Agosti 21, 2019 fidia zote zimeshalipwa na hakuna mwananchi anayedai.

Mkurugenzi huyo amemjulisha Nyongo kwamba kwa sasa  kampuni husika inafanya matengenezo ya barabara na miundombinu mingine na itakapofika Oktoba 2019, ianze ujenzi wa mitambo.