Majeruhi ajali gari la Tanapa wahamishiwa Bugando, Arusha

Muktasari:

Majeruhi sita kati ya 18 wa ajali ya gari la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lililopinduka eneo la Lamai Wilaya ya Tarime wakati wakitoka kuzima moto wamehamishiwa Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha na ile ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.

Serengeti. Majeruhi sita kati ya 18 wa ajali ya gari la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lililopinduka eneo la Lamai Wilaya ya Tarime wakati wakitoka kuzima moto wamehamishiwa Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha na ile ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.

Muuguzi mkuu wa Hospitali Teule ya Nyerere wilaya ya Serengeti, Neema Binagi amewataja waliohamishiwa Bugando kuwa ni ni Kurwa Mwamanda (30), Mrigo Mewama (28) aliyevunjika mkono wa kushoto, Baraka Joseph (32) aliyepata mtikisiko wa kichwa na Petro Michael aliyevunjika mkono wa kushoto.

Waliohamishiwa hospitali ya Mount Meru ni Ayubu Kimani (22) aliyevunjika kiuno na Petro Buyoya (31) aliyevunjika mguu wa kushoto.

Kamanda wa Polisi  Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema ajali hiyo ilitokea jana Agosti 20, 2019 kutokana na utelezi baada ya mvua kubwa kunyesha wilayani Tarime.

Amesema majeruhi wa ajali hiyo ni John Kely, Emmanuel Christian, Mgaya Maguye, Samwel Kuhurwe, Lushinge Ndonge, Mathias David, Kelvin Molel na Joel Wilshayo na kwamba walitibiwa katika zahanati ya Seronera na kuruhusiwa baada ya kubainika kutokuwa na madhara makubwa.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amewapa pole majeruhi na kubainisha kuwa uchunguzi wa kina wa sababu za ajali hiyo utafanywa na polisi wilayani Tarime kulikotokea ajali.