Maandamano yamuumiza kichwa Rais wa Malawi, sasa kuingiza jeshi

Muktasari:

Rais wa Malawi, Peter Mutharika ametangaza kupeleka vikosi maalumu vya jeshi katika mipaka yote pamoja na viwanja vya ndege ili kuwadhibiti waandamanaji.


Lilongwe, Malawi. Rais wa Malawi, Peter Mutharika ametangaza kupeleka vikosi maalumu vya jeshi katika mipaka yote pamoja na viwanja vya ndege ili kuwadhibiti waandamanaji.

Uamuzi wa Rais Mutharika umekuja muda mchache baada ya waandamanaji nchini humo kutangaza kufanya mfululizo wa mikutano ya hadhara nchini kote sambamba na kufunga kiwanja cha ndege.

Jumatano iliyopita vikundi vya upinzaji na asasi za kiraia vinavyopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Mutharika vilitangaza kufanya maandamano makubwa yenye lengo la kuvuruga utoaji wa huduma katika maeneo muhimu ikiwamo viwanja vya ndege na katika mipakani ya nchi hiyo kuanzia siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, Rais Mutharika alisema atachukua hatua zote muhimu za kutetea nchi hiyo kutoka kwa wale wanaotaka kuchukua madaraka kwa nguvu kutoka kwake.

Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa hali ya usalama nchini Malawi imezidi kudorora baada ya Chama cha upinzani cha Malawi Congress (MCP) kinachoongozwa na Lazarus Chakwera kupinga hatua ya kuchaguliwa tena kwa Rais Mutharika.

Mara kwa mara polisi nchini humo wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji wanaongozwa na viongozi wa juu wa vyama vya upinzani.

Vyama hivyo pia vimefungua kesi katika Mahakamani Kuu ya Malawi kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini humo na kutaka mwenyekiti wa tume hiyo kujiuzulu.

June 6, balozi wa Marekani nchini Malawi, Virginia Palmer alishambuliwa na mabomu ya machozi akiwa katika ofisi za makao makuu ya chama cha upinzani wakati polisi walipokuwa wakirusha mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji waliokuwa nje ya jengo hilo.