Polisi wataja sababu kuwashikilia wanachama wa ACT-Wazalendo

Kamanda wa Polisi Temeke, Amon Kakwale

Muktasari:

Jeshi la Polisi wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Tanzania limesema linawashikilia wanachama watatu  wa  ACT-Wazalendo na mwandishi wa habari kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Tanzania limesema linawashikilia wanachama watatu  wa  ACT-Wazalendo na mwandishi wa habari kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.

Jana  Jumamosi Agosti 24, 2019 polisi walizuia mkutano wa ndani wa chama hicho uliokuwa ufanyike wilayani humo.

Waliokamatwa ni katibu wa uadilifu, Mbarala Maharagande; mwenyekiti wa jimbo la Ilala, Mwikizu Mayama; mwenyekiti wa chama hicho Temeke, Said Mohammed na mwandishi wa habari wa televisheni mtandao ya Gillybon, Haruna Mpaunda.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Agosti 25, 2019  Kamanda wa Polisi wilayani humo, Amoni Kakwale amesema waliokamatwa walikuwa wakiongoza maandamano bila kuwa na kibali.

"Kama unataka taarifa zaidi unaweza kufika ofisini mimi nakupa taarifa kama msemaji,  waliokamatwa walikuwa wakifanya maandamano kinyume na sheria,” amesema Kakwale.

Alipoulizwa sababu za kukamatwa kwa mwandishi wa habari amesema hawezi kutofautisha mwandishi na mwanachama, wote wanahojiwa kwa kosa moja.

"Mimi sio ninaowahoji nakupa taarifa tu wote wamekamatwa kwa kosa moja wewe ndio unaweza kutofautisha mwandishi na mwanachama,” amesema.

Katibu wa oganaizesheni na mafunzo wa chama hicho, Sheweji Mketo amesema wanaendelea kufuatilia ili wanachama wao wapatiwe dhamana.

Kabla ya mkutano huo kuzuiwa baadhi ya viongozi waliokuwa wamefika ni mshauri mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.