Kesi ya kina Dk Tenga, Mahakama yatoa siku 14 upande wa mashtaka kuwasilisha nyaraka

Wednesday August 28 2019

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Tanzania, imetoa siku 14 kwa upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo watano wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili maarufu Dk Ringo Tenga, kuhakikisha unawasilisha nyaraka muhimu Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Ufisadi.

Dk Tenga  ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa Kampuni hiyo na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh8 bilioni ).

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Agosti 28, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Simba amesema kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika, hivyo upande wa mashtaka unatakiwa kuhakikisha una kamilisha kazi ya kuwasilisha nyaraka muhimu Mahakama Kuu ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kwamba wanaomba siku 14 ili waweze kukamilisha kazi ya kuwasilisha nyaraka muhimu Mahakama Kuu.

Advertisement

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Novemba 20, 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Katika kesi ya msingi, Dk Tenga na wenzake wanadai kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani  0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya TCRA kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Vilevile katika kipindi hicho, washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh.8bilioni ).

 


Advertisement