Lissu: Nasubiri ruhusa ya madaktari kurejea Tanzania

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema hatarejea Tanzania Septemba 7, 2019 kama ilivyopangwa badala yake atasubiri ruhusa ya madaktari wanaomtibu.

 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema hatarejea Tanzania Septemba 7, 2019 kama ilivyopangwa badala yake atasubiri ruhusa ya madaktari wanaomtibu.

Lissu ametoa kauli hiyo jana Jumanne Septemba 3, 2019 katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), alipoulizwa lini atarejea Tanzania.

Amesema  bado madaktari hawajaweka bayana kwamba atarudi lini.

 “Sio bayana maana daktari wangu hajaniambia bado kwamba sasa nenda nyumbani, hajaniambia bado,” amesema Lissu aliyefungua maombi ya kuomba kufungua kesi kupinga kuvuliwa ubunge.

Lissu, amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa eneo la makazi yake Area D, Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali akiwa hajitambui kisha usiku wa siku hiyo alisafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Lissu alitibiwa Nairobi mpaka Januari 6, 2018 kisha alihamishiwa nchini Ubelgiji ambako yupo mpaka sasa akipatiwa matibabu.

Kauli aliyoitoa BBC ni tofauti na aliyoitoa Mei 23, 2019 alipoeleza sababu mbili za kuitumia siku ya Jumamosi ya Septemba 7, 2019  kurejea nchini baada ya kuwa nje kwa miaka miwili huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema maandalizi ya ujio huo yameanza.

Mwanasiasa huyo aliyefanyiwa upasuaji zaidi ya mara 20 katika hospitali zote tatu za Dodoma, Nairobi na Ubelgiji alieleza sababu ya kurejea nchini Septemba 7. “Madaktari wangu wamenipa ahadi ya kukutana nao Agosti 20 na baada ya hapo nitapata ruhusa, sasa baada ya hapo nitakuwa nasubiri kuonana nao kila mwaka.”

Pili, alisema “Septemba 7 niliondoka Tanzania nikiwa nusu mfu, kuna watu walitaka nife hivyo nimeamua Septemba 7 iwe safari yangu ya kurudi Tanzania nikiwa mzima ili kudhihirisha hao waliotaka kuniua kuwa niko hai.”

Sababu hizo mbili ziliungwa mkono na Mbowe aliyesema Septemba 7 ni siku muhimu na maalumu kwa wapigania demokrasia na haki za binadamu.