VIDEO: Meno ya Tembo yalifukiwa humu

Muktasari:

Ni baada mtaani kwao kukamatwa nyara za Serikali

Dar es Salaam. Siku kadhaa baada shehena ya meno na pembe za ndovu kukamatwa zikiwa zimefukiwa ndani ya nyumba, majirani waliokuwa wakiishi jirani na nyumba hiyo wameonyesha kushangazwa na tukio hilo.

Juzi waziri wa maliasili na utalii kwa kushirikiana na maofisa wa serikali kupitia kikosi cha Taifa cha kuzuia ujangili kilikamata vipande 338 vya meno ya Tembo vyenye dhamani ya shilingi 4 Bilioni na 40 Milioni nyumani kwa Hassan maarufu Nyoni.

Mwananchi ilifika katika mtaa wa Mkondogwa eneo ilipo nyumba hiyo ambayo zilikamatwa nyara hizo za serikali.Ni nyumba ya iliyozungushiwa ukuta, ndani ya ukuta kuna uwanja mdogo ambao hutumika kuegesha gari.

Kwenye uzio kuna vifaa vingi vya magari ambavyo vinaonekana kuwa vibovu na vikuukuu vinavyoonekana kama uchafu.

Pembezoni mwa ukuta kuna shimo linalokadiriwa kuwa na urefu wa futi saba hadi saba na nusu ambalo ndilo kulikofukiwa meno hayo.

Mmoja wa majirani katika eneo hilo, Ali Ngemba alieleza kuwa ameishi hapo kwa muda mrefu na ameshangazwa na taarifa za ujangili huo kufanyika mtaani kwake.

Alieleza kuwa alikuwa akimfahamu mtuhumiwa kwa kumuona lakini hafahamu shughuli zake kwa sababu hakuwa mtu wa kuonekana mtaani mara kwa mara.

“Huyu mtu tulikuwa tunamuona akipita mtaani kwenye gari yake, hakuwa mtu wa kujichanganya na wenzie na maisha yetu jinsi yalivyo hapa mjini ni vigumu kujua mtu anafanya nini hadi akwambie mwenyewe,”

“Kiukweli tukio hili limetushangaza majirani na kuzua taharuki mambo haya yanafanyikaje na inawezekana vipi mtu kuwa na mzigo wote ule nyumbani kwake,imetuletea doa kubwa,” alisema Ngemba

Jirani mwingine ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake kwa sababu za kiusalama alisema alimfahamu mtuhumiwa huo kwa zaidi ya miaka mitatu aliyokaa mtaani hapo lakini hakufahamu shughuli zake.

“Anapita pale kwangu anapiga honi ananisalimia lakini si mtu wa kujumuika, pale kuna kijiwe cha kahawa au kuna sehemu nyingine wanaume huwa tunakutana mara kwa mara lakini yeye huwezi kumuona,

“Sifahamu shughuli zake ila nasikia anahusika na magari sasa sifahamu hayo magari anaendesha, anauza au anakodisha, mkewe ndiye huwa anakaa hapo nje jirani na wanawake wenzie,”

Hata hivyo majirani wengi waliofuatwa kwa ajili ya mahojiano walikataa kuzungumza wakihofia usalama wao.

“Unaambiwa mtu amekuta na mzigo wa mabilioni sasa unafikiri hiyo ni kitu kidogo, lazima ni mtandao sasa leo nianze kumzungumzia mtu wao, waje wanifuate najali maisha yangu,”

Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mkondogwa Shabani Miyombo alieleza kuwa tukio hilo limewaamsha kuanza kuwaangalia kwa jicho la ukaribu wageni wanaokwenda kwenye mtaa huo.

Alisema, “Tumepata fedheha na imeleta taswira mbaya kwa mtaa wetu, mie nilifika eneo la tukio siku polisi walipofika kiukweli nilijikuta nashangaa, mzigo mkubwa vile wa nyara za serikali kuwa nyumbani kwa mtu,”

“Ni ngumu kufahamu kila mtu hasa hawa wapangaji lakini kwa hili kuna haja ya kujipanga upya tuwaelekeze mabalozi kuwafuatilia wananchi wao huko kwenye mitaa yao maana mzigo kama ule haiwezekani kuwa umeingia kwa siku moja,”alisema

Juzi Waziri wa maliasili na utalii Dk Hamisi Kigwangla alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akikusanya meno ya tembo kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani ya msumbiji.

“Amekuwa akihangaika kutafuta na meno hayo kutafuta soko kwa miaka minne bila mafanikikio kutokana na wateja kubaki sisi wenyewe” alisema

Alisema idadi ya vipande hivyo vilivyokamatwa 338 ni sawa na idadi ya tembo 117 waliowindwa ambapo pia kuna meno mawili ya kiboko.