Mugabe aliipenda Tanzania na Afrika, mengine tumwachie Mungu

Sunday September 8 2019Robert Mugabe.

Robert Mugabe. 

By Luqman Maloto

Mtoto halisi wa Afrika, Robert Mugabe, hatimaye amelala usingizi wa dawamu. Miaka 95 aliyoishi duniani, kwa hakika Mungu alimwezesha kuishi muda mrefu na amefanya mambo mengi.

Sikitiko ni kuwa Mugabe amefia Singapore. Taswira ileile ya viongozi wa Afrika kutojenga mifumo mizuri ya huduma za afya kwenye nchi zao na kuishia kuwa wakimbizi wa mataifa mengine pale wanapotekwa na magonjwa.

Mugabe alikuwa Kiongozi wa Serikali (Waziri Mkuu) kuanzia mwaka 1980 mpaka 1987 na kuanzia mwaka 1987 alipoondolewa Rais Canaan Banana, aliyekuwa mkuu wa nchi, Mugabe alikuwa Rais mwenye mamlaka yote, mkuu wa Serikali, mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu.

Mugabe aliondolewa madarakani mwaka 2017. Mpaka wakati huo, alikuwa amekaa madarakani kwa miaka 37 – Miaka saba kama mkuu wa Serikali na 30 akiwa na mamlaka yote. Pamoja na hivyo, amefia Singapore alipokuwa anatibiwa.

Kitendo cha Mugabe kufia Singapore ni nyongeza ya dharau kuwa Waafrika hakuna wanachoweza. Zaidi ya miaka 62 tangu Uingereza iliporidhia kuipa Ghana uhuru wake ikiwa ya kwanza, kisha kuibua vuguvugu la kudai Uhuru wa kikatiba kila kona, bado Waafrika hawajiwezi katika huduma za afya. Viongozi wake ni wakimbizi wa matibabu ughaibuni.

Miaka 29 tangu nchi ya mwisho Afrika, Namibia, ipate uhuru, viongozi wa Afrika wanatibiwa ughaibuni na watoto wao wanasoma Ulaya na Marekani.

Advertisement

Afrika Kusini ambayo ilipata uhuru haramu mwaka 1912, kwa Wazungu kuchukua mamlaka yote na kuwabagua watu weusi, mwaka 1994, wakati utawala wa kidemokrasia unapatikana, nchi ilikuwa na mifumo bora ya afya, shule na vyuo.

Leo Afrika Kusini ni kimbilio la Waafrika kwa matibabu na utafutaji wa maisha mpaka kuibua mapigano ya chuki kati ya wenyeji na wageni. Unafuu ambao Waafrika wanaufuata Afrika Kusini, ulijengwa wakati wa Serikali ya kikaburu.

Miaka 10 ya kuondoka kwa Serikali ya kikaburu Afrika Kusini, dunia ilishuhudia nchi hiyo ikikumbwa na ufisadi mkubwa wa ununuzi wa silaha uliomhusisha aliyekuwa Makamu wa Rais, Jacob Zuma, kisha baadaye ikashuhudiwa marais wake wawili wakilazimishwa kujiuzulu kwa kashfa mbalimbali.

Mambo yenye kuendelea Afrika, kisha Mugabe ambaye amekuwa alama ya utetezi wa heshima ya Bara la Afrika, kufia ughaibuni, yanapunguza ujasiri wa kuwabishia Wazungu wanaposema Waafrika hawakuwa tayari kujitawala.

Viongozi wao ni wezi, wanajitajirisha kihuni badala ya kujenga nchi. Wengine madikteta, hawaheshimu Katiba, ving’ang’anizi wa madaraka wanaotaka nchi iende kwa utashi wao.

Usaliti ni mkubwa ndani ya Afrika na viongozi wake. Manung’uniko ya nchi na nchi yanafanya Waafrika waonekane ni kichekesho cha dunia.

Katika eneo la ung’ang’anizi wa madaraka, unamkuta Mugabe. Mungu amemchukua, lakini atabaki kuwa alama ya wazi ya viongozi wa Afrika, kung’ang’ania uongozi, hata pale wanapojiona wameshindwa.

Muongo wa pili ukielekea tamati Karne ya 21, milenia ya tatu, Afrika ndilo bara ambalo viongozi wake wanaendelea kuchezea Katiba ili wabaki madarakani. Wanachezea Bunge na Mahakama watakavyo. Ndilo bara ambalo viongozi wanaendelea kupinduliwa na wananchi au jeshi. Mugabe aliipenda Tanzania na Afrika, mengine tumwachie Mungu!

Nchi yake ikadidimia, ikawa mufilisi

Mambo mawili ambayo ni hakika kwa Watanzania ni kuwa Mugabe aliipenda Tanzania na aliihusudu Afrika. Alijivunia kuwa Mwafrika na alitamani kuona Waafrika wanakuwa na msuli dhidi ya Wazungu.

Kingine ni kwamba Mugabe alikuwa mwenye shukurani. Siku zote alitambua mchango wa Tanzania katika kuikomboa Zimbabwe na nchi nyingi za Afrika.

Mugabe alimpenda na alimheshimu Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere. Kitabu chake “Julius Nyerere, Asante Sana, Thank You Mwalimu” kinabeba sauti kubwa yenye utii na shukurani, iliyokuwamo ndani yake kuhusu Mwalimu Nyerere na Tanzania.

Ndani ya kitabu hicho, Mugabe anakiri kuwa Mwalimu Nyerere aliingia gharama kubwa kuikomboa Afrika, akiwa taa ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU), vilevile Mwalimu alifanya makao makuu ya Kamati Maalum ya Ukombozi Afrika, kuwa Dar es Salaam, Tanzania.

Mugabe alieleza kukumbuka nyakati bora za wapigania ukombozi Afrika kuishi Tanzania na kuweka kambi za mafunzo ili kujiandaa vema kwenda kuzikomboa nchi zao. Mugabe aliandika kuwa Tanzania ilibeba mzigo wote wa Afrika.

Alieleza mengi kuhusu Nyerere na Watanzania. Alisema ushirikiano wa Nyerere na China, ndio uliojenga ushirikiano wa Afrika na China, kwani Nyerere hakutaka Tanzania pekee ifaidike kwa urafiki huo, bali bara zima.

Swali, Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere, ilipigania uhuru wa nchi ngapi? Ni viongozi wangapi walioandika vitabu kushukuru na kukumbuka mchango wa Mwalimu? Mugabe alikuwa mwenye shukurani.

Alipenda Mwalimu Nyerere atambulike kuwa baba wa ukombozi Afrika, na alionyesha wazi furaha yake, siku lilipopitishwa wazo kuwa jengo la Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, lipewe jina la Mwalimu Nyerere.

Hivyo, kuna mengi ambayo Mugabe aliyafanya. Kwa wenye kuamini malipo ya matendo ya mja duniani huanza baada ya kifo chake, basi ya Mugabe aachiwe Mungu, jaji wa mwisho, lakini hapaswi kusahaulika kwa namna alivyoipenda Afrika, Tanzania na alivyomtukuza Mwalimu Nyerere.

Lala salama Jongwe, Robert Mugabe!

Advertisement