VIDEO: Mbowe: Maombi ya Lissu yamekataliwa, tunajipanga tutarejea mahakamani

Mbowe asema watarejea mahakamani baada ya maombi ya Lissu kukataliwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema baada ya Mahakama Kuu kukataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma, watarejea tena mahakamani baada ya kushauriana.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wanajipanga  kurejea mahakamani baada ya leo Jumatatu Septemba 9, 2019 Mahakama Kuu ya Tanzania kukataa, Tundu Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha apoteze sifa za kuwa mbunge wa Singida Mashariki.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo baada ya Jaji Sirillius Matupa kutoa uamuzi huo, kubainisha kuwa Lissu hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Jaji Matupa amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Mbowe amesema mahakama ni chombo wanachokiamini wamesikia uamuzi wa Jaji, watarejea tena katika mahakama hiyo, “Ndugu yetu Lissu bado yuko nje ya nchi kwa matibabu tutafanya mawasiliano katika chama tutaendelea kutafuta haki hadi ipatikane.”

"Tunatambua haitapatikana kwa urahisi kwa sababu mbalimbali ila maamuzi yaliyotolewa kama chama tunayaheshimu. Mahakama ni chombo muhimu cha kutoa haki tutaendelea kutumia kila mfumo kuhakikisha haki inatendeka.”

Ameongeza, “Katika mahakama kuna ngazi mbalimbali za kupata haki tutaendelea kutumia kila mfumo  wa mahakama  kuhakikisha haki hiyo inaendelea kupiganiwa na kutafutwa.”

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na mahakama iteunge taarifa hiyo.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.