VIDEO:Polisi Tanzania watekeleza amri ya Lugola kumkamata Nabii Mahela

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola atembelea kanisa la Pentecostal Power Ministries na kaamuru Nabii wa kanisa hilo kukamatwa na kushtakiwa baada ya kuvunja sheria ikiwemo kuwapigia kelele majirani.

Dar es Salaam. Nabii wa Kanisa la Pentecostal Power Ministries nchini Tanzania, Nabii Elia Mahela amejikuta akidondokea mikononi mwa polisi  baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Kangi Lugola kufanya ziara katika kanisa hilo lililopo maeneo ya Kimara Temboni wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.

Nabii Mahela anatuhimiwa kukaidi sheria za nchi, ikiwemo kanisa kupiga kelele kinyume cha taratibu hali inayosababisha kero kwa majirani wanaozunguka eneo hilo.

Uamuzi wa kukamatwa kwa Nabii Mahela umetolewa leo Jumatatu Septemba  9, 2019  na Waziri Lugola baada ya kufanya ziara katika kanisa hilo kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa majirani dhidi ya kanisa hilo.

Amesema majirani wa eneo hilo kwa nyakati tofauti wamekuwa wakilalamika kelele zinazotoka kanisa hilo na licha ya viongozi wa Serikali kumpa onyo la kujirekebisha mchungaji huyo hakufanya hivyo.

"Ulikuwa ukiwaambia wananchi kuwa ujali na waende kokote leo kokote zimefika 40. Kokote nipo hapa na kokote hutopona," amesema Lugola.

Awali, baadhi ya majirani ya kanisa hilo, wamemweleza Lugola kuwa mchungaji wa kanisa hilo amekuwa na tabia ya kuweka ‘flash’ yenye nyimbo mbalimbali na kufungulia sauti kubwa bila kuwepo mtu kanisani.