Wajane wa waliokufa ajali ya moto Morogoro waomba msaada

Muktasari:

Wajane wa waliokufa katika ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro wameiomba Serikali ya Tanzania kuwawezesha mikopo ili waweze kuanzisha biashara ndogo ili kutunza familia walizoachiwa na waume zao.

Morogoro. Wajane wa waliokufa katika ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro wameiomba Serikali ya Tanzania kuwawezesha mikopo ili waweze kuanzisha biashara ndogo ili kutunza familia walizoachiwa na waume zao.

Wanawake hao, Mariam Mziwanda na Salma Jafari  walifiwa na waume zao katika ajali hiyo iliyotokea Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Wakizungumza na Mwananchi jana Jumatatu Septemba 16, 2019, Salma amesema mumewe pamoja na mume wa Mariam walikuwa ndugu, akisisitiza kuwa kwa sasa anakaribia kujifungua na hajui maisha yatakuwaje.

Salma amesema tangu alipofariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikohamishiwa akitokea Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, anaishi kwa wakwe zake, wamekuwa wakitegemea misaada ya watu mbalimbali.

Naye Mariam amesema mumewe alikuwa akifanya biashara ndogo katika eneo ilipotokea ajali hiyo, amemuacha na watoto sita ambao wanahudumiwa na mama mkwe.

Amesema walifanikiwa kujenga nyumba na mumewe lakini haijamalizika, kuomba Wasamaria wema kumsaidia kumaliza nyumba hiyo aweze kuishi na watoto wake.

Akizungumza matunzo ya wanawake hao, mama wa marehemu hao, Shida Said amesema alikuwa akiwategemea watoto wake, ila baada ya kufariki yeye ndio amebeba jukumu la kuisaidia familia.

“Hawa wajane wako kwenye eda kwa muda wa miezi mitatu na siku 10 na hawawezi kutoka kujitafutia mpaka muda huo upite hivyo mimi nalazimika kuwa mhudumiaji wa familia kwa kutegemea kuomba misaada kwa ndugu na jamaa,” amesema Shida.