Samatta: Nilitamani kucheza soka Ulaya nikiwa chini ya miaka 18

Mbwana Samatta 

Muktasari:

Ushawahi kujiuliza nini ambacho Mbwana Samatta anatamani kingetokea katika maisha yake. Mwenyewe amesema alitamani kucheza soka barani Ulaya akiwa na umri chini ya miaka 18.


Dar es Salaam. Mbwana Samatta ameeleza jinsi alivyotamani kucheza soka barani Ulaya akiwa na umri mdogo zaidi.

Mchezaji huyo wa klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji ameeleza hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, kwamba ingekuwa vyema angeanza kucheza soka barani humo akiwa na umri chini ya miaka 18.

“Tujadili kidogo ni jambo gani unatamani lingetokea katika maisha yako mapema? Mimi natamani ningekuwa katika soka la Ulaya kabla hata sijafika miaka 18. Hatukosoi mipango ya Mungu,” amesema Samatta katika ujumbe wake huo.

Swali hilo liliibua mjadala ambapo 66_dIIh amesema, “Mimi pia Mbwana Samatta ningekuwa kama wewe.”

Agathadastorywriter  ameandika, “Mimi natamani kila mtu ajue uwezo wangu wa kuandika simulizi ambazo zinagusa maisha ya watu …Still waiting for God’s ryt time.”

Hivi karibuni Samatta ameandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufunga goli kwenye michuano hiyo.

Rekodi ya Samatta iliibua furaha kwa Watanzania, ingawa iligubikwa na matokeo mabaya ya klabu yake kupoteza mchezo wake wa kwanza kwa kufungwa mabao i 6-2 na RB Salzburg.

Msimu uliopita alifunga jumla ya mabao 32 katika mashindano yote,  23 ya Ligi Kuu Ubelgiji na tisa katika michuano ya Europa.

Alijiunga na KRC Genk Januari 29, 2016 akitokea TP Mazembe ya DRC Congo ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, aliondoka Afrika akiwa na tuzo ya uchezaji bora kwa wachezaji wa ndani.

Katika dirisha la usajili mwaka 2019,  Aston Villa na Leicester City zinazoshiriki Ligi Kuu Uingereza ziliweka mezani Pauni 12 milioni kumsajili Samatta lakini zilikataliwa na klabu yake iliyotaka Pauni 15 millioni.