VIDEO: Mtoto wa Mabeyo aliyekufa kwenye ajali ya ndege alitarajia kuajiriwa ATCL

Muktasari:

  • Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Ladislaus Matindi amesema Nelson Mabeyo, mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance  aliyefariki katika ajali ya ndege jana Jumatatu Septemba 23, 2019 alikuwa rubani mtarajiwa wa shirika hilo.

Dar es Salaam. Nelson Mabeyo, mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance  Mabeyo aliyefariki katika ajali  ndege alikuwa akitarajia kuajiriwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Hayo yameelezwa  leo Jumanne Septemba 24, 2019 na mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi.

Nelson alikuwa rubani katika ndege ya kampuni ya Auric Air iliyoanguka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania.

Ndege hiyo ilianguka jana saa 1:30 asubuhi wakati ikipaa katika uwanja huo kwenda mkoani Arusha. Nelson aliondoka na ndege hiyo juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JINA), Dar es Salaam na wakati akipata ajali alikuwa na rubani mwanafunzi, Nelson Orutu ambaye pia amefariki.

 “Nelson alikuwa ni rubani mzuri na alishika nafasi ya pili katika usaili  wetu,  na marubani 16 waliajiriwa na ATCL hivi karibuni. Alikuwa aondoke mapema kwenda Canada kwa ajili ya mafunzo ya kurusha Bomberdier ila aliomba amalizie mkataba wake na mwajiri wake (Auric),” amesema Matindi.

Matindi amesema Nelson alikuwa rubani mzuri na mwenye umri mdogo.