Profesa Tibaijuka kurejesha Sh1.6 bilioni za mgawo wa Rugemarila

Muktasari:

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Profesa Anna Tibaijuka amesema uongozi wa Shule ya Sekondari Barbro Johansson Model Girls utarejesha  fedha walizopokea kama msaada kutoka wa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemarila.

Dar es Salaam. Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amesema uongozi wa Shule ya Sekondari Barbro Johansson Model Girls utarejesha fedha za msaada walizopokea  kutoka kwa mfanyabiashara, James Rugemarila ili aweze kutoka gerezani.

Profesa Tibaijuka amesema hayo leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 kupitia Kituo cha televisheni cha Azam UTV.

Amesema uongozi wa shule hiyo umekaa kikao na kuamua kurejesha  fedha hizo walizopokea ili kumsaidia  mtuhumiwa huyo anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kutoka gerezani.

“Suala hili sio langu binafsi maana fedha hizi ni za shule, mwenyekiti wangu (wenyekiti wa bodi), Salmon Odunga na mwenyekiti wa wazazi, Dk Kiharuzi wamekaa kwenye kikao wakaamua fedha zirudi."

"Nashukuru kwa msimamo huo kwa kuwa ndio msimamo wangu pia kwamba kama itasaidia, tunashukuru Mungu," amesema Profesa Tibaijuka.

Alipoulizwa kama fedha walizopewa msaada zilikuwa hazijatumika hadi sasa,  Profesa Tibaijuka amesema licha ya fedha hizo kutumika kulipa deni la kujenga bweni la shule lakini zitatafutwa na zitarejeshwa.

“Fedha zenyewe zilikwenda kulipa deni la mkopo ambao tulijenga bweni lakini taasisi kama hii inapoamua kurejesha fedha zitatafutwa na kurejeshwa” amesema.
 
Amesema kutokana na Rais wa Tanzania, John Magufuli kushauri  watuhumiwa wa uhujumi uchumi waandike barua kukiri na kurejesha fedha na mali,  wao watarejesha kiasi walichopewa na Rugemarila.

 “Msamaha wa Rais unapotoka ni fursa adimu, sasa fursa ukiichezea utabaki kujuta mwenyewe, kwa upande wangu na  shule, sisi tunashughulika na ule mchango tulioupokea tunaurudisha mezani” amesema profesa Tibaijuka.

Profesa Tibaijuka alipokea mchango wa Sh1.617 bilioni kutoka kwa Rugemarila ambazo amesema zilitumika kwa ajili kulipa mkopo waliokuwa wakidaiwa katika Bank M.

Rugemarila anakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.