Nigeria yapitisha muswada wa kuzuia unyanyasaji wa kingono kwa wanafunzi

Muktasari:

Muswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza katika seneti ya Bunge hilo jana Jumatano Septemba 9, unapendekeza kifungo cha kati ya miaka mitano na miaka 14 kwa wahadhiri ambao wana uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wao.

Lagos. Nigeria. Serikali ya Nigeria imewasilisha bungeni muswada wa sheria ya kuzuia vitendo vya unyanyasaji kingono kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Muswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza katika seneti ya Bunge hilo jana Jumatano Septemba 9, unapendekeza kifungo cha kati ya miaka mitano na miaka 14 kwa wahadhiri ambao wana uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wao.

Hatua hiyo inafuatia ripoti ya Shirika la Utangazaji (BBC), iliyofichua vitedo vya unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wahadhiri wengi katika vyuo vikuu viwili vikuu vya Afrika Magharibi.

Katika taarifa yake, Naibu wa Rais wa seneti ya nchi hiyo, Ovie Omo-Agege alisema ana matumaini uchunguzi wa BBC utasaidia kuongeza msaada katika muswada wake.

“Kama baba, unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo vikuu ni suala ambalo siwezi kulikubali,” alisema seneta Omo- Agege.

Ikiwa muswada huo utapitishwa utazuia wahadhiri kuwa na uhusiano na wanafunzi wao hata kama ni wa hiari.