Ndani ya boksi: Katikati ya Mondi na Kiba kuna fursa

Sunday October 20 2019

 

‘Gemu’ liko wazi kama vazi la kahaba, huhitaji kuchungulia. Yeyote akiamua atasimama pale juu na kuwa namba moja. Na hili ndilo tatizo kuu la muziki. Masikio yana ujinga wa kupenda kitu. Yanakomalia mpaka kiishe utamu wake. Baadaye yanakitosa jumla. Yanaanza kutafuta kingine mbadala cha kusikia.

Mwaka wa 10 huu anasikika Diamond tu. Huku mitaani wapo wengi lakini kwa wingi alisikika Diamond tu. Hata kwenye timu ya mpira kuna wachezaji wengi, lakini siyo wote nyota. Diamond ndiye nyota wa mchezo kwa miaka 10 tangu atoke kisanii 2009. Hili halihitaji ubishi kwa sababu namba hazidanganyi.

King Kiba ni kama alilisusa ‘gemu’. Kisha ghafla akaibuka na kuleta upinzani kwa Mondi. Kwenye hili Kiba na Mondi hawakuwa washindani. Bali WCB walishindana na Team Kiba. Kifupi ni kwamba ‘Team Kiba’ na WCB ndo wahanga wa kila kitu kuliko Kiba na Mondi mwenyewe. Walikuza mambo zaidi ya uhalisia.

Mashabiki wa King Kiba wanampenda yeye kuliko muziki wake. Hata alipotoa ngoma mbovu walisimama naye na kutetea kana kwamba haikuwa ridhaa yake kuzitoa. Lakini namba haziongopi baada ya kutoka na ngoma ya ‘Mwana’, ‘Aje’ na ‘Seduce Me’ Kiba hajatoa ‘hits songs’ zaidi ya hizo. Zipo zingine lakini siyo ‘hits songs’.

Kwa maana nyingine Kiba na Mondi ushindani wao uliwasaidia wote kibiashara. Mondi katoa nyimbo nyingi nyepesi lakini zilikuzwa na fujo za WCB ili kuzima ngebe za Kariakoo, ndo maana nyimbo kubwa za Mondi ni za kipindi kile. Hivi karibuni katoa nyingi zenye maisha mafupi kama ya funza. Fuatilia.

Kuna kitu watu hawajaona au wameamua kutoona, Mondi akifanya ngoma kivyake ni tofauti na akishirikishwa na madogo zake. Kwenye ngoma ya ‘Kwangwaru’ utadhani dogo kabebwa. Hapana, ila ukubwa wa jina la Diamond unambeba zaidi ya muziki wake. Ndivyo ilivyo dunia nzima. Kwake kila kitu kinaenda sawa kikiwa kimeganda pale pale.

Advertisement

Kuna sehemu Mondi kaganda na masikio yanataka kitu kipya ‘Nyegezi’, ‘Tetema’ ni ngoma za Rayvnny zilizotikisa kuliko ‘Kanyaga’ na nyinginezo za Mondi. Hapa tuelewane. Mondi hajachuja bali masikio yanahitaji kitu kipya unadhani Joe Thomas hawezi tena kuimba? Yuko vizuri tu na ubora wake tatizo nyakati.

Unapomuona Koffi Olomide, akitisha wakati anaitafuta 70. Heshimu hilo jambo. Lady Jaydee bado ana sauti na mwonekano na utunzi uleule, tena hivi sasa ana ufundi zaidi kadri umri unavyosogea.

Lakini si yule wa miaka 10 iliyopita na si kwamba kaisha bali muziki ndivyo ulivyo masikio yanahitaji kitu kipya kila siku.

Ladha rafiki na masikioni ya sasa ni sauti na matukio ya Nandy, Ruby na madem wengineo. Inasikitisha ukatili wa masikio kuitenga hata sauti ya Ndege Mnana Linnah. Masikio yamevunja undugu na Ray C, Mwasiti na wenzao. Si kwamba hawatoi ngoma wanatoa bila mwitikio kama ule wa zamani.

Harmonize anaanzaje kutaka kukaa kando ya mbavu za Simba wa Tandale? Muda huu unaruhusu yeyote awe. Kwa sababu ‘gemu’ liko wazi kama utupu wa kahaba. Liko tayari kuolewa na yeyote. Posa yako ni ngoma kali zaidi. Bahati mbaya wanamuziki wengi wanavizia Fiesta. Hawajiamini.

Mbali na masikio kutaka kitu kipya, jambo ambalo ni la kidunia. Pia Kibongo Bongo tuna tabia ya kutaka kuona mtu mpya. Hatutaki kumuona yuleyule hata kama anafanya vizuri zaidi ya jana. Ndipo hulazimisha upinzani na mwingine ili kumuondoa mtu kwenye reli. Ni kama utani ila zama zimefika tamati.

Mtazame Chameleone wa Uganda anaendelea kutoa ngoma kwenye ubora, sauti ile ile na ana fedha lakini mapokeo ya watu kwake si kama wakati ule. Alipotoa ngoma Afrika Mashariki ilisimama. Ngoma moja ingemtengenezea mamilioni ya fedha hapa Bongo hata mara tatu kwa mwaka.

Angeitwa kwenye Fiesta angepewa tuzo ya Kill ya msanii/wimbo bora wa Afrika Mashariki. Angetumbuiza Miss Tanzania lakini kwa muda mrefu alizimwa kabisa na uwepo wa Mondi na Kiba. Huko kwao kwenyewe hawa madogo walipiga fedha kwenye vibaraza vya mama zake. Mashabiki walimkatia laini.

Masikio ya watu yalikosa ‘linki’ na sauti ya Chameleone si yeye tu wasanii wakubwa wengi hupitia hii hali duniani. Sasa ni wakati wa mtu kama Mondi kujikita kwenye uwekezaji, kama aliingiza mguu mmoja katika miradi sasa aweke miguu miwili kibabe zaidi. Muziki hauna wastaafu ila hauna urafiki wa kudumu.

Harmonize hakustahili hata kujaribu kumtikisa Mondi lakini bila shaka kwa jicho la kawaida unaona ngome ya WCB imetikiswa. Uzito wa kuondoka kwa Rich Mavoko si sawa na Harmo hakuna makeke wala mbilinge. Lakini mitaani tukio lake ni zaidi ya Mavoko alipoondoka, umelielewa picha hapo?

Daraja la Mondi ni kubwa sana lakini mtikisiko wa kuondoka kwa Harmo iwe kama taa kwake kushtuka kwamba hata D B’anji wa leo si kama wa juzi. Lakini anaendelea kuingiza fedha kutokana na uwekezaji wake ndivyo ilivyo kwa wanamuziki kama R Kelly bado ni mnyama lakini si yule.

Wale Rostam muunganiko wao umezalisha kitu kipya wamekuwa wapya. Masikio ya watu yanataka kuwasikia kwa sababu ni ladha mpya ambayo bado haijaanza kukinai masikioni, ingawa nao ni waviziaji wa Fiesta. Bila shaka wanafuata upepo hawana ‘gatsi’ za kuamrisha upepo uende wanavyotaka.

Hili la kusubiri ‘shoo’ za jumuiya nalo ni tatizo kubwa, nyimbo zinatolewa kwa msimu kama sikukuu za Pasaka, Xmass na Eid. Yaani mwaka unapokaribia kuisha ndipo wanaachia ngoma wanavizia ‘shoo’ za jumuiya hawawezi mpaka walundikwe kwenye kapu moja.

Hili si kosa la wasanii peke yake. Kungekuwa na Tuzo za Kill, wasingesubiri ‘shoo’ za jumuiya, kungekuwa na Miss Tz yenye nguvu wangetoa nyimbo ‘deile’. Bahati mbaya hata ‘mapromota’ mikoani hawapo wametoweka kama kunguru wa doa jeupe Daslama mjini. Hakuna mchongo.

Jide alituhamisha kwenye vijiwe vyetu mpaka Victoria (Ghounzhou). Akatupeleka Thai Village Masaki, kisha Nyumbani Lounge Namanga. Alikuwa juu licha ya shida alizopitia akili hiyo aliipata ili aende sawa na soko la wakati huo. Hakutegemea tena ‘shoo’ za Matei Lounge Dom wala La Casa Chica Tanga.

Lakini kabla ya hapo Jide aliishi kwa ‘shoo’ na mauzo ya albamu. Kwa sasa msanii kama Mondi hahitaji kupiga ‘shoo’ kila wiki ni kuwekeza zaidi kwenye miradi. Huu si wakati wa ‘drama’ za madem tena kwake. Hatutengenezi Mr Nice mpya tunamtaka Oliver Mutukuzdi, Angelique Kidjo na Youssou N’Dour wa kwetu.

Kama tunazalisha mastaa masikini tutakaa kimya lakini tukitengeneza wenye utajiri mkubwa tutasema tu. Walikaa kimya kwa kina Mr Nice sisi hatuwezi kukaa kimya kwa Mondi hatutaki kuwa na staa aliyepanga Mbezi Beach wala kuacha masikio ya watu yamkinai.

Hata kama hupati kingi lakini Harmo kuachana na WCB ni zaidi ya ujasiri. Hata kama ni kwa wema bado mamilioni ya mashabiki wa Mondi vigumu kukuelewa. Kwa nini Konde Boy kajiamini na kusepa? Ameona nini? Mbele kuna mema zaidi ya mabaya? Harmo si mwehu. Hii inatoa picha kuwa ‘gemu’ liko wazi kwa sasa ndo maana dogo kaamini anaweza kutengeneza fedha nje ya WCB. Kuna tundu liko wazi tatizo watu tunaishi kwa mazoea na kukariri katikati ya Mondi na Kiba kuna fursa, ukiitumia unapasua kwa kuwa sababu masikio yamekinai kuwasikia wawili tu.

Advertisement