RC Chalamila ampa saa 24 DED kuhamisha ofisi

Monday October 21 2019

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ametoa saa 24 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Steven Katemba kuhamisha makao makuu ya ofisi yake kutoka katikati ya Jiji la Mbeya zilizopo hivi sasa na kuzihamishia mahali popote ndani ya mipaka ya halmashauri yake.

Chalamila ametoa agizo hilo leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo alichokiitisha kwa dharura kusilikiza mapendekezo ya madiwani hao wanakopendeza kupeleka makao makuu ya halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania John Magufuli la kuzitaka halmashauri zote zihamie kwenye maeneo ya mipaka yake.

Hivi sasa Ofisi za Halmashauri za Wilaya ya Mbeya, zipo katikati ya Jiji la Mbeya.

Amesema kufikia kesho Jumanne asubuhi mkurugenzi huyo awe amehamisha ofisi hizo na kuzipelekea popote wanapotaka kulingana na mapendekezo ya madiwani hao.

“Mkurugenzi kesho asubuhi uondoke hapa ulipo, utakwenda wapi sijui... Lakini gari la magereza, gari la Polisi na gari la Jeshi yapo tayari kuhamisha nyaraka za Serikali,” amesema

“Mahali mnataka kuweka wapi makao makuu yenu sijui lakini ninachotaka kesho mhamishe ofisi zenu.”

Advertisement

“Hivyo hapa ninataka nisikilize mapendekezo yenu na mkishindwa kufikia muafaka mimi nitatoa uamuzi wa wapi halmashauri ipelekwe,” amesema

Madiwani hao wanaendelea kutoa mapendekezo ya wapi halmashauri yao ipelekwe.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Advertisement