TCRA yawapa mbinu Wasioona kukabiliana na utapeli kwa njia ya simu

Monday October 21 2019

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imekutana na watu wasioona mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwapatia elimu ya mawasiliano huku wakitakiwa kutumia vyema huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kusajili laini za simu kwa alama za vidole.

Ofisa wa kitengo kinachoshughulika na wateja na watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano kutoka TCRA, Wolter Marick akizungumza leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 jijini hapa, amesema ni haki kwa kila mtumiaji wa mawasiliano kupata elimu hiyo.

“Rai yangu kwa watumiaji ni kwamba, tuwe makini tunapotumia hizo huduma za mawasiliano, mawasiliano yana vitu vingi lakini changamoto ya uelewa wa utumiaji wakati mwingine inakuwa shida kwa baadhi ya wanaotumia tofauti na malengo yaliyokusudiwa,” amesema Marick.

 

Amesema Serikali inaendelea na kazi ya  usajili wa laini kwa alama za vidole, hivyo ametoa rai kama bado hawajafanya hivyo, wakasajili sasa.

Hata hivyo, amesema licha ya kuwa wameendelea kutoa elimu kwa wateja wao, lakini walipata barua ya maombi kutoka chama cha watu wasioona wakiomba kupatiwa mafunzo.

Advertisement

 “Mfano kwenye kutumia huduma za mawasiliano hasa kwenye fedha, mtu anapokea ujumbe mfupi kutoka kwenye namba fulani kuwa ameshinda bahati nasibu ili hali hajawahi kushiriki mashindano hayo, tunawataarifu kuwa msitekeleze maagizo mtakayoambiwa,” alisema.

Mwenyekiti wa chama cha watu wasioona Mkoani Dodoma, Omary Lubuva amesema katika makundi yanayoweza kuathirika kwa urahisi kwa kutokuwa na taarifa za kutosha kama kwenye mitandao ya simu ni watu wasioona.

Hivyo, amesema elimu hiyo imekuwa chachu kwao hivyo wataongeza umakini wakati wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwa namna tofauti.

Advertisement