Wakiri makosa, watakiwa kulipa Sh300 milioni

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu  Donald Njonjo na mfanyabiashara wa Tandika sokoni, Gamba Muyemba kulipa fidia ya Sh300 milioni baada ya kukiri kosa la kuuza madini bila kibali.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu  Donald Njonjo na mfanyabiashara wa Tandika sokoni, Gamba Muyemba kulipa fidia ya Sh300 milioni baada ya kukiri kosa la kuuza madini bila kibali.

Njonjo ambaye ni meneja ukaguzi wa shughuli za maabara Wizara ya Madini na mwenzake wamehukumiwa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina.

Hakimu huyo aliamuru washtakiwa hao kulipa Sh50 milioni leo, jambo ambalo walilitekeleza.

Kiasi kilichobaki cha Sh250 milioni, washtakiwa hao  wanatakiwa kukilipa kwa awamu ndani ya miezi 12 kuanzia leo.

Pia, mahakama hiyo imetaifisha mali za mshtakiwa Donald ambazo ni viwanja viwili  ploti namba 51/1/bloc C kilichopo  Njedengwa high Density Dodoma na kingine kilichopo eneo la Nzuguni B Dodoma.

Vingine vilivyotaifishwa ni gari aina ya Nissan Hard Body na kwamba vyote vitakuwa  mali ya serikali.

Mahakama hiyo pia imetaifisha madini feki ya dhahabu feki yenye uzito wa kilogramu 2,794.5.

Hakimu Mhina amesema kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni na iwapo watashindwa watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.