MCT yakemea vyombo vya habari visivyochukua tahadhari

Katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga

Muktasari:

Baraza la Habari Tanzania (MCT) linakemea baadhi ya vyombo vya habari vya kimapokeo na mtandaoni vinavyoandika habari bila tahadhari.

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) linakemea baadhi ya vyombo vya habari vya kimapokeo na mtandaoni vinavyoandika habari bila tahadhari.

Imesema habari hizo zinatokana na matamshi yanayochochea chuki au taarifa za uongo na zenye lugha ya kuudhi.

Katika taarifa ya baraza hilo iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 na katibu mtendaji wake, Kajubi  Mukajanga inaeleza kuwa endapo hali hiyo ikiachwa inaweza kuleta uhasama mkubwa baina ya viongozi na wananchi au makundi mengine ya kijamii kama ilivyowahi kutokea katika nchi za Kenya na Rwanda.

“Tunavitaka vyombo vya habari kuzingatia maadili na weledi vinaporipoti kauli za viongozi wa kisiasa, kidini, kijamii au za wapambe wao ili visije kugeuzwa vipaza sauti au wapiga debe.”

“Kwa sababu kumeibuka vyombo vya habari vinavyoitwa ‘vya kimkakati’ vilivyojikita kuandaa na kusambaza taarifa zinazochochea chuki, vikitumia lugha zisizofaa kinyume na utamaduni wa Mtanzania na matakwa ya taaluma, bila kujali athari zinazoweza kujitokeza,” inaeleza taarifa hiyo.

Kutokana na hilo MCT imewataka wahariri kutoingia katika mtego wa kuwa vipaza sauti vya kupitishia matamko ya  kuchochea chuki na uhasama, au taarifa ambazo hawajajiridhisha kuwa ni za kweli.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa matamko ya chuki yanapaswa kuripotiwa kwa tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuepuka ushabiki na kubainisha madhara ya matamko hayo.

“Siyo kazi ya vyombo vya habari kutoa taarifa za  uongo na kupaka watu matope,  na badala yake vyombo vya habari vizingatie maadili ya taaluma ambayo yanawataka kudhibiti au kupunguza madhara katika habari kabla haijamfikia msomaji au msikilizaji.”

“Tunakemea kwa nguvu zote suala hili hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020. Vyombo vya habari vya Tanzania vikatae kushiriki katika mradi wowote wa kuchochea uhasama katika Taifa kwa kusambaza uzushi, matusi, vitisho, na chuki,” inaeleza taarifa hiyo.