CCM yapita bila kupingwa wilaya tatu Dodoma, wagombea Chadema waendelea

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Muktasari:

Wilaya tatu za Kongwa, Chamwino na Kondoa mkoani Dodoma nchini Tanzania hazitapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 baada ya wagombea wote Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa. 

Dodoma. Wagombea wote wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye wilaya za Chamwino, Kondoa na Kongwa mkoani Dodoma nchini Tanzania wamepita bila kupingwa.

Akizungumza jijini Dodoma leo Jumatano Novemba 20, 2019 Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Jamila Yusuph amesema katika maeneo mengine ya wilaya za Dodoma Mjini, Mpwapwa, Chemba na Bahi wamejitokeza wagombea wa vyama vingine.

Amewataja wagombea waliojitokeza ni Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na  Chama cha Wakulima (AAFP).

“Mbali na CCM, Wilaya ya Bahi kata ya Kigwe kuna wagombea wa chama cha NCCR- Mageuzi pamoja na CUF, Wilaya ya Dodoma Mjini kuna chama cha AAFP, Wilaya ya Mpwapwa kuna Chadema na Wilaya ya Chemba kuna chama CUF pamoja na Chadema,” amesema Jamila.

Hata hivyo,  amesema Mkoa wa Dodoma una Vijiji 564 kati ya hivyo 533 sawa na asilimia 94 CCM wamepita bila kupingwa.

Amesema mitaa 255 kati ya  258 sawa na asilimia 98 CCM imepita bila kupingwa wakati vitongoji 3,117 kati ya 3,210 sawa na asilimia 97 wamepita bila kupingwa.

Amewataka wanachama kutobweteka kwa kufurahia ushindi huo bali waendelee kutafuta ushindi katika maeneo yaliyobaki kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili chama hicho kishinde kwa kishindo.

“Pia hatuna mashaka na uchaguzi mkuu mwakani kwani uchaguzi huu wa serikali za mitaa unatupa taswira ya uchaguzi ujao utakuwaje hivyo tuna imani hautakuwa na kazi kubwa lakini haitufanyi tubweteke,” amesema.

Kwa upande wake, Wilaya ya Dodoma Mjini CCM imepata washindani kutoka chama cha AAFP katika mitaa ya Njedengwa West, Chihikwi na Chadulu B