Mtifuano Chadema uchaguzi wa kanda

Dar/mikoani. Wabunge wa Chadema ni miongoni mwa wagombea waliopitishwa na kamati kuu kuwania uongozi wa chama hicho ngazi ya kanda.

Kanda hizo 10 za Chadema zitafanya uchaguzi kabla ya Desemba 10 ili kutoa fursa ya uchaguzi wa chama hicho ngazi ya taifa ambao utafanyika Desemba 18.

Kanda hizo ambazo wagombea wake wametajwa ni Pwani, Kaskazini, Kusini, Nyasa, Pemba, Unguja, Katavi, Magharibi, Serengeti na Kanda ya Victoria.

Nafasi zinazowaniwa kwenye uchaguzi wa kanda hizo ni pamoja na Mwenyekiti, Makamu na Mweka Hazina,

Mchuano mkali unatarajia kuwa kanda ya Kaskazini ambapo wabunge Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joseph Selasini wa Rombo wamepitishwa kuwania uenyekiti.

Nafasi ya Makamu mwenyekiti ni Jaffar Koimere, Yosepher Komba (Mbunge Viti Maalum), Emmanuel Landey na Jonathan Bahweje wakati nafasi ya Uhazini ni Pricar Michael, Anna Gidarya (Mbunge wa Viti Maalum), Bahati Mollel na Salim Mphare.

Mchuano mwingine utakuwa Kanda ya Serengeti, wabunge; Esther Matiko (Tarime Mjini) na John Heche wa Tarime Vijijini watachuana na wagombea wengine Mshemasi Yakobo na Alex Malima kuwania uenyekiti.

“Nimejipanga vizuri kabisa, mimi nilikuwa mwenyekiti wa kanda, ninaomba tena kuchaguliwa, mimi ni kiongozi mzoefu lakini hiki ni chama cha kidemokrasia kila mtu ana haki ya kugombea na huu mchuano ndio uhai wa chama.

“Ukiangalia kila sehemu ushindani ni mkali sana na hii ni dalili chama kinakuwa na nguvu na kina watu wenye uwezo, kwa hiyo ni uchaguzi mgumu,” alisema Heche.

Mbunge wa Viti Maalum, Gimbi Massaba, King Tarai, Jackson Luyombya watachuana kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti na wanachama wanne wanawania Uhazini.

Wanaowania nafasi hiyo ni Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Ruge, Maendeleo Makoye, Pascalia Sanya na Meshack Kajila.

Taarifa ya juzi ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi ilionyesha kuwa ni kanda moja ya Pwani ambayo itakuwa na mgombea pekee, ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye anayewania uenyekiti.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Baraka Mwago, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Ruth Mollel na Waziri Mwenevyale wakati uhazini ni Florence Kasilima, Joseph Zahabu na Michael Mtaly na Omary Mkama.

Majina ya wagombea hao yalipitishwa na kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichoketi Novemba 23.

Mwita aliishukuru kamati kuu kwa kumpitisha akisema; “Ninakwenda kupambana na vigogo katika mchakato huu nina imani nitashinda kwa sababu si mgeni ndani ya Chadema. Nikishinda nitaongeza nguvu mkoa wa Pwani.”

Mwago anayegombea nafasi moja na Mwita alisema akishinda atahakikisha anawaunganisha wanachama wa Chadema wa Dar es Salaam na Pwani.

Wagombea waliohojiwa walitaja vipaumbele ambavyo wanatarajia kuvifanya ni pamoja na kuiimarisha Chadema ili iwe ni taasisi imara ya kisiasa.

Vipaumbele vingine vilivyotajwa na wagombea hao ni kuunganisha wanachama, kuhakikisha chama kinajitegemea na kila wilaya kuwa na ofisi.

Kanda nyingine na nafasi wanazowania kwenye mabano ni Unguja ambao ni Salim Mzee Saidi (mwenyekiti), Hassan Abeid, Alawi Alawi (makamu mwenyekiti) na Asiata Abubakari (mhazini).

Nyingine ni Pemba, Hafidh Ali Saleh, Hassan Husein, Omary Nassoro (mwenyekiti), Alawy Hamad, Time Suleiman (makamu mwenyekiti) na Ali Khamis Ali na Seif Ali Hatibu (mweka hazina).

Kanda ya Magharibi ni Ngassa Ganja Mboje, Gaston Shundo Garubindi (mwenyekiti), Masanja Katambi (makamu mwenyekiti) na Idan Laurent Ndowa anawania nafasi ya mweka hazina.

Kusini wamo Cecil Mwambe, Mansa Nyuchi, Seleman Kuwongo, Willy Mkapa (mwenyekiti), Mahadhi Mmoto, Salum Barwan (makamu), Mario Millinga na Zubeda Sakuru (mweka hazina).

Kanda ya Nyasa ni mchungaji Peter Msigwa, Sadick Malila, Boniface Mwambukusi (mwenyekiti), Sophia Mwakagenda, Fadhili Mwaya na Joseph China (makamu mwenyekiti).

Katika kanda hiyo, Susan Mgonokulima na Aidan Khenani wanawania nafasi ya mweka hazina.

Kanda ya kati ni Alphonce Mbassa, Lazaro Nyalandu (mwenyekiti), Shaba Mikongollo, Imelda Malley, Dk Albanie Marcossy (makamu mwenyekiti), Devotha Minja ambaye ni mbunge Viti Maalum na Tully Kiwanga (mweka hazina). Kanda ya Victoria ni Andronicus Chief, Ezekiah Wenje, Clorence Njugu (mwenyekiti), Sylvester Makanyaga, Peter Mutagahywa (makamu) na Sijaona Karolina Upendo Peneza (mweka hazina).

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Jesse Mikofu (Mwanza), Nazael Mkiramweni (Dodoma), Haika Kimaro (Mtwara) na Juma Mtanda (Morogoro), Bakari Kiango, Fortune Francis (Dar es Salaam)