Mbunge CCM ataka majina waliouziwa ardhi

Mbunge wa Handeni Mjini (CCM) nchini Tanzania, Omari Kigoda

Muktasari:

Mbunge wa Handeni Mjini (CCM) nchini Tanzania, Omari Kigoda ameagiza kupelekewa majina ya waliopewa maeneo na kufanya shughuli za kilimo katika malisho la mlima Mkuzi.

Handeni. Mbunge wa Handeni Mjini (CCM) nchini Tanzania, Omari Kigoda ameagiza kupelekewa majina ya waliopewa maeneo na kufanya shughuli za kilimo katika malisho la mlima Mkuzi.

Amesema hata kama ni viongozi ni vyema majina hayo yakapelekwa ili kufahamu wamepata kwa njia gani.

Kigoda ametoa kauli hiyo leo Jumatano Desemba 4, 2019 katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi kata ya Kwamagome.

Katika ziara hiyo amekutana na  kundi la wafugaji waliomlalamikia kuwa wananyanyaswa na kunyimwa uhuru wa kufuga huku wakiwatuhumu viongozi kuuza maeneo bila kufuata utaratibu.

"Mimi siogopi, naagiza nyie wenyeviti (wa Srikali za mitaa) mkutane na kuniorodheshea watu wote wanaolima huko kwenye eneo la malisho.”

“Kibali cha kulima humo wamepewa na nani wakati kuna pingamizi (makahamani), pia kuna amri ya mkuu wa wilaya aliyepita Husna Msangi kuwa njia za mifugo zifunguliwe mbona hakuna kilichofanyika," amesema Kigoda.

Mwenyekiti wa wafugaji wilaya ya Handeni, Paul Matema amesema hatua za haraka zisipochukuliwa kuthibiti mambo yanayoendelea katika msitu huo wa malisho kunaweza kutokea ugomvi kwa kuwa wafugaji watachoka kuvumilia.

Diwani Kwamagome, Mussa Mkombati amesema suala hilo lipo mahakamani na wanasubiri majibu ili kutatua kero hiyo ambayo ni kubwa katika kata yake.