Kampuni ya Bia Tanzania yataka ETS itumike simu za mkononi

Muktasari:

“Ni muhimu kwa masoko yetu, kwa sababu mfumo huu utasaidia kupambana tatizo la bidhaa bandia katika biashara yetu.”

Dar es Salaam. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imependekeza kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikiria matumizi ya Stempu za Kielektroniki (ETS) kwenye matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya kufuatilia bidhaa sokoni.

Mkurugenzi mtendaji wa TBL, Philip Redman alisema jana kuwa ETS ni mfumo mzuri unaotoa nafasi ya kulinganisha kati ya wingi wa bidhaa na kodi inayolipwa.

Redman alisema katika awamu ya kwanza, walianza kutumia ETS katika bidhaa za vileo na baadaye waliweka katika bidhaa za Grand malt kama walivyoshauriwa na TRA.

Alisema kampuni yake imeweka mfumo huo kwenye bidhaa zake na katika awamu ya kwanza, walianza kutumia ETS katika bidhaa za vileo na baadaye ilipokuja awamu ya pili, wameweka katika bidhaa za Grand malt kama walivyoshauriwa na TRA.

Serikali ilitangaza mpango wa kutumia mfumo huo tangu Juni mwaka uliopita  na unafungwa na Kampuni ya Uswisi -Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA).

Kampuni hiyo iliingia mkataba wa kuweka mitambo yake na kusaidia mfumo wa mtandao na mitambo kwa ajili ya mfumo huo.

“Tunafurahi sisi kuwa moja ya kampuni za mwanzo kutumia ETS Tanzania,” alisema Redman.

“Ni muhimu kwa masoko yetu, kwa sababu mfumo huu utasaidia kupambana tatizo la bidhaa bandia katika biashara yetu,” alisema.

Hata hivyo, Redman alisema kulikuwa na changamoto ya makubaliano ya matumizi ya mfumo huo kwa vipindi vifupi wakati wa uzalishaji.

Alisema kushuka kwa ETS kulisababisha kusimama kwa kazi na kusimamisha uzalishaji.

“Gharama kubwa ya wino unaotumika ulichangia kwa kiasi kikubwa hasa katika pombe kali kwa mfano, wakati bei ya Stemp ikiwa Sh46 badala ya bei ya awali ya Sh7 kwa stempu moja,” alisema redman.

Awamu ya kwanza ya ETS ilianza Januari 15, 2019, mfumo huo uliwekwa kwenye kampuni 19 zinazozalisha vileo, mvinyo na pombe kali.

Awamu ya pili ilianza Agosti Mosi, 2019, kwa kuweka stempu hizo katika vinywaji baridi na vile vyenye kaboni na maji ya chupa.

Mfumo huo unaiwezesha Serikali kung’amua upotevu wa mapato zaidi kama ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya mapato.

 

Naibu Kamishna wa TRA, Msafiri Mbibo anasema mamlaka hiyo inafanya juhudi ili kuhakikisha kila bidhaa inayozalishwa inawekewa mfumo huo.

Alisema mfumo huo umelenga kuondoa uwezekano wa kufurika kwa bidhaa zisizo na ubora sokoni.

“Tumejipanga kuweka uwanja sawa kwa wazalishaji wote,” alisema Mbibo.