Ulinzi ulivyoimarishwa maadhimisho ya Uhuru Tanzania

Muktasari:

Leo Jumatatu Desemba 9, 2019 kunafanyika maadhimisho ua Uhuru wa Tanganyika jijini Mwanza nchini Tanzania ambapo ulinzi umeimarishwa ndani na nje ya uwanja.

Mwanza. Unashangaa watu kuujaza uwanjani wa CCM Kirumba Mwanza nchini Tanzania tangu saa 10:00 alfajiri kuwahi tukio la maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru?

Basi ukifika na kushuhudia jinsi ulinzi ulivyoimarishwa utashangaa hadi ujishangae mwenyewe jinsi ulivyoshangaa.

Kwa lugha ya soka, ulinzi wa leo Jumatatu Desemba 9, 2019 ndani na nje ya uwanja wa CCM Kirumba wenye uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 25,000 unaweza kuitwa ni ulinzi wa mtu kwa mtu. Hakuna kupeana gepu!

Yaani kila anapokanyaga raia, basi askari aidha wa Jeshi la Polisi, Magereza, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwenye sare na aliyevaa kiraia naye anakanyaga kwa mtindo wa mtu kwa mtu katika mchezo wa Soka.

Hivyo ndivyo mtu unavyoweza kuelezea hali ya ulinzi na usalama ulivyoimarishwa ndani na nje ya uwanja wa CCM Kirumba ambao tayari ‘umetapika’ watu kwa jinsi ulivyojaa.

Akizungumzia ulinzi huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema “Kifupi vikosi vyote viko timamu kutekeleza jukumu la ulinzi na usalama kwenye tukio hili kubwa la Kitaifa na Kihistoria,”

“Wapo askari wanaoonekana kwa macho kutokana kuvaa sare na vivyo hivyo waliovaa kiraia. Yote ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda na kumaliza salama,” ameongeza Kamanda Muliro

Ukaguzi milangoni

Wingi wa askari pekee siyo ndiyo inawahakikishia usalama viongozi na wananchi wanaohudhuria maadhimisho hayo, bali pia kuna ukaguzi ‘wa kufa mtu’ kwa kutumia mitambo maalum ya usalama kabla mtu yeyote kuruhusiwa kuingia uwanjani.

Hakuna asiyekaguliwa. Wote wanakaguliwa bila kujali vyeo, mamlaka na madaraka yao.

Kwa viongozi wa kada mbalimbali wanakaguliwa katika eneo maalum lililotengwa katika viwanja vya Rock city mall ambako pia wameandaliwa kifungua kinywa kabla ya kupanda mabasi madogo yanayowaingiza moja kwa moja uwanjani.

“Viongozi wote wanakaguliwa Rock city mall ambako pia wanapata kifungua kinywa na kupanda magari maalum kuingia uwanjani; atakayeshuka kutoka kwenye gari atalazimika kukaguliwa tena mlangoni kabla ya kuruhusiwa kuingia,” hayo ni maelekezo ya Katibu Tawala mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio kwa viongozi wenzake

Hakuna kurandaranda uwanjani

Siyo kukaguliwa pekee, bali hata baada ya kuingia uwanjani, kila mmoja anaelekezwa pa kukaa na hakuna ruhusa ya kutembea tembea au kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Waandishi wa habari na wapiga picha miongoni mwa makundi yenye majukumu uwanjani hapo ambao pia wamepewa maelekezo maalum ya jinsi ya kukaa na kutekeleza majukumu yao bila kuingilia majukumu na taratibu zingine.

Huko mitaani ni shwari

Kuimarika kwa ulinzi hakujaonekana ndani na nje ya uwanja wa CCM Kirumba pekee, bali hata katika mitaa ya jiji la Mwanza ulinzi umeimarishwa kwa kuwepo doria ya magari na miguu kila eneo la jiji la Mwanza.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi