VIDEO: Mufuruki alivyoona kifo chake

Muktasari:

Ali Mufuruki, aliajiriwa kwa muda mfupi kabla na baada ya kuhitimu shahada ya uhandisi mitambo (mechanical engineering) kutoka Chuo Kikuu cha Reutlingen nchini Ujerumani, tangu hapo amekuwa ni mjasiriamali aliyeipigania sekta bin-afsi Tanzania.

Tangu mwaka 1989 alipoanzisha kampuni ya Infotech Investment Group mpaka leo, aliendelea kuwa ofisa mtendaji mkuu na mwenyekiti.Ndani ya kampuni hiyo, alimiliki kampuni nyingine kadhaa zilizoji-husisha na biashara ya masuala tofauti ikiwamo lnfotech Computers aliyoanza nayo mwaka huo.Baada ya miaka sita (1994), alian-zisha kampuni ya mawasiliano aliy-oiita M&M Communication na miaka mitano baadaye (1999) akafungua kampuni ya W-Stores inayouza nguzo za chapa ya Woolworths ikiwa na matawi Dar es Salaam na Arusha pamoja na Kampala, Uganda.

Mwaka 2006 alianzisha kampuni ya majengo ijulikanayo kama Info-tech Place ikiwa na ofisi jijini Dar es Salaam na Geita.Mufuruki alizaliwa Novemba 15, 1958 wilayani Bukoba na kusoma Shule ya Msingi Katerero, alihitimu mwaka 1971 kisha akajiunga na Sekondari ya Lake (1976) jijini Mwanza kabla hajaenda Old Moshi alikohitimu mwaka 1978.

Kukamilisha uzalendo, alikuwamo kwenye operesheni Kagera mwaka 1978.Hakuaminiwa ndani tu, amefariki akiwa mdhamini wa Chuo cha Mandela (Minds) Afrika Kusini na mwenyekiti mwenza wa kamati maalumu ya Bunge la Uingereza ya kuchunguza manufaa ya misaada yake kwa nchi za Afrika.

Dar es Salaam. Safari ya bilionea Ali Mufuruki ilihitimishwa jana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, lakini shughuli hiyo ikitawaliwa na maneno ya busara, hisia na kumbukumbu za saa za mwisho za mfanyabiashara huyo maarufu.

Kati ya salamu nyingi za rambirambi zilizotolewa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jana, kumbukumbu zilizovuta hisia za wengi ni zile zilizotolewa na Zuhura Muro kuelezea alichokisema Jumamosi saa chache kabla ya kuhamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

“Leo nitaanza kwa kutoa neno la faraja. Na katika kutoa neno la faraja, nitazungumzia muda wa mwisho niliokuwa nao na kaka yangu, rafiki yangu na mwalimu wangu Ali Mufuruki,” alisema Zuhura mkurugenzi mkuu wa Lindam Group Limited mbele ya umati wa wafanyabiashara, viongozi wa kampuni, mabalozi na viongozi wa taasisi mbalimbali.

“Hiyo ilikuwa ni mapema Jumamosi asubuhi, saa za asubuhi wakati wote tulipokuwa tukihangaika kumpeleka Afrika Kusini. Niliamka asubuhi na kwenda moja kwa moja hospitalini kumtembelea.

“Alikuwa amefumba macho. Nilinyanyua mkono wake wa kulia na nilikuwa nasali. Na mara alipogundua nilikuwa pembeni ya kitanda chake nikisali, alifungua macho yake na akaniambia kwa njia ileile aliyokuwa amezoea kuniita; ‘Zu, naelekea kufa’.

“Nilimwambia ‘Ali hutakufa. Umepigana vita mara nyingi ukashinda, utashinda na hii’. Akasema ‘hapana, hapana. Nataka kwenda’.”

Zuhura, ambaye alisema aliamua kutumia lugha ya Kiingereza kwa sababu alifanya kazi na Mufuruki katika nchi za Afrika Mashariki, alikuwa akisema hayo huku ukumbi ukiwa umetulia na kumsikiliza kwa makini. Baadaye alisoma shairi linaloelezea siku kifo kinapokuja na kwamba watu wasiogope kwa kuwa katika dini ya Kiislamu kifo ni huruma ya Mungu.

Alisema amejifunza mengi kutoka kwa Mufuruki lakini kikubwa ni upendo, uadilifu na uchapakazi wake kwa jamii, watoto wake na mke wake, Saada Ibrahim.

Zuhura alisema Mungu ameamua kumchukua Mufuruki kwa kuwa amekamilisha kile alichomtuma na kila mmoja atajifunza kutoka kwa yale aliyoyafanya kuwaomba kuendelea kumwombea.

Alikuwa mmoja wa wazungumzaji wengi waliovuta hisia za wasikilizaji, huku baadhi wakishindwa kujizuia na kububujika machozi.

Amliza bosi TPSF

Mmoja wa waliojikuta wakibubujika machozi ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye.

Huku akitokwa machozi, Simbeye alisema Mufuruki amefariki dunia kabla hajafanikiwa kumshawishi kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.

“Mufuruki amekuwa kwenye bodi nyingi lakini kuna kitu hajakifanya na nilitamani akifanye lakini hakijatokea,” alisema Simbeye huku akishindwa kuendelea kuzungumza kwa sekunde kadhaa na macho yake akiyaelekeza kushoto kwake ulipokuwa umelazwa mwili wa Mufuruki

Alisema TPSF ilitamani mfanyabiashara huyo awe mwenyekiti wake, kwamba licha ya kumfuata na kumueleza mara kwa mara alijibu kuwa haikuwa muda wake.

“Nilimuuliza kuwa anatamani kuwa mwenyekiti wa TPSF akasema ndio ila kwa sasa ngoja kwanza Mzee Reginald Mengi (marehemu) aendelee,” alisema.

Simbeye alisema juhudi zake hazikuishia hapo na hakukata tamaa.

Naye kaimu mwenyekiti wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, Magreth Ikongo alisema Mufuruki alikuwa mtu wa kusikiliza nini mtu anasema.

“Wengi tunakosa sifa ya kusikiliza lakini yeye hata katika mikutano ya wanahisa alikuwa anaruhusu maswali na kuyajibu inavyostahili,” alisema.

Wengine waliotoa salamu zao ni mabalozi wa nchi tofauti.

Mabalozi wamlilia

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier alisema Mufuruki alikuwa mtu wa pekee aliyeweza kubadilishana utaalamu wake na wafanyabiashara na wakuu wa nchi.

Alisema mfanyabiashara huyo alikuwa mzalendo kwa Tanzania na bara zima la Afrika.

“Katika maisha yangu nimekutana na watu wachache aina ya Mufuruki. Alikuwa akisaidia vijana kukua kibiashara. Mchango wake utaendelea kuishi ndani ya vijana wengi,” alisema balozi Clavier.

Naye Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook alisema Mufuruki alikuwa rafiki mkubwa wa nchi yake na walifanya kazi kwa ushirikiano na kushauriana mambo mbalimbali.

Alisema Mufuruki alikuwa na mawazo ya kujenga na wakati mwingine alitoa changamoto kwa mambo ambayo hakubaliani nayo lakini kwa lengo la kujenga.

“Ali alikuwa rafiki wa ajabu, alikuwa anakuja nyumbani tunaongea na kushauriana mambo mbalimbali,” alisema balozi Cook.

“Tumepoteza rafiki ambaye tulifanya naye kazi kwa karibu, tulimuamini sana.”

Kaimu balozi wa Marekani, Dk Inmi Patterson alieleza jinsi Tanzania ilivyopoteza mtu mwenye kujali maendeleo ya Watanzania na Taifa.

Alisema Mufuruki ni mfano wa kuigwa kwa kuwa licha ya familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha, alipambana mwenyewe kwa kujisomesha hadi kufikia hatua aliyofikia.

“Mara ya mwisho kuonana alinipa kitabu cha maono ambacho kilibeba matumaini yote ya Watanzania na kinaonyesha jinsi alivyo mkarimu na mwenye moyo mwema. Mufuruki nitakukumbuka na Watanzania watakukumbuka pia,” alisema.

Ilichokisema Serikali

Katika hafla hiyo ya kuaga mwili wa Mufuruki, Serikali iliwakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki na naibu katibu mkuu ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Joseph Sokoine.

Waziri Kairuki alisema Mufuruki alikuwa akisimamia anachokiamini hata kama ni tofauti na wengine walichokiamini kwamba lengo lake lilikuwa ni kuona sekta binafsi inakua.

“Serikali itaendelea kumuenzi Mufuruki kwa maneno na vitendo hasa kusikiliza maoni kutoka sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini,” alisema Kairuki.

Alisema Serikali inatambua mchango wake katika kukuza uchumi kwa kutengeneza ajira kwa wananchi kupitia kampuni yake ya Infotech Investment na Woolworths na kulipa kodi serikalini.

Kampuni ya NMG, MCL

Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ya Kenya na Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Tanzania zimesema zitamkumbuka Mufuruki kwa mchango wake katika kampuni hizo.

Kampuni hizo zimesema Mufuruki alishiriki kwa uwezo wake kuijenga MCL na waandishi wake ambao wengine wamekwenda kuajiriwa maeneo mengine.

Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa bodi ya MCL, Leonard Mususa wakati akitoa salamu za rambirambi za MCL na baadaye kusoma ujumbe wa mwenyekiti wa bodi ya NMG, Wilfred Kiboro.

Enzi za uhai wake, Mufuruki aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya MCL, ambayo ni kampuni tanzu ya NMG inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mitandao yake ya kijamii.

Mususa alisema licha ya kuwa na umri mdogo, alikuwa akijifunza mengi kutoka kwa Mufuruki kutokana na uwezo aliokuwa nao.

“Yeye ndiye aliyenijenga na yeye alisaidia kujenga sekta ya habari. Wapo waandishi wengi wametoka Mwananchi na kwenda kuajiriwa kwingine,” alisema Mususa.

“Pale Mwananchi ukiongea na kila mtu bado wanaheshimu mchango wake, alikuwa anaendelea kuchangia katika magazeti yetu kwa fikra chanya.

“Mwananchi tumesikitika sana kwa msiba huu, sijui tutapata mtu kama yeye ila kwa kuwa amewajenga wengi tutampata.”

Akisoma ujumbe wa Kiboro, Mususa alisema NMG itamkumbuka Mufuruki kwa uwezo wake, kufanya kazi kwa kujituma, kuwafundisha wengine. Kifo chake ni pigo kubwa si kwa Tanzania pekee bali hata nje ya Tanzania.

Alisema Mufuruki ametoa mchango mkubwa kwa NMG.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Peter Elias na Asna Kaniki