DC Sabaya azuia fedha za mfuko jimbo la Mbowe, ampa maagizo DED

Muktasari:

Shule ya Mijongweni iliyopo kata ya Mnadani haina choo cha walimu kwa muda mrefu na walimu wamekuwa wakijisaidia katika choo cha Zahanati iliyopo jirani na shule.

Moshi. Mkuu wa wilaya ya Hai (DC) mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya, amezuia Sh42 milioni za mfuko wa Jimbo la Hai na kuagiza kati ya fedha hizo Sh7 milioni ziende kujenga choo cha walimu wa shule ya msingi Mijongweni iliyopo kata ya Mnadani wilayani humo.

Fedha hizo za mfuko wa Jimbo hilo linaloongozwa na Mbunge wake, Freeman Mbowe kupitia tiketi ya Chadema, zilikuwa zigawanywe kwa kila kijiji ambapo katika mgawanyo huo, kila kijiji kingepewa Sh500,000.

Hata hivyo, Sabaya amesema leo Jumamosi Desemba 28,2019 kuwa ametoa maagizo kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai, Yohana Sintoo, kutoa Sh7 milioni na kuzipeleka katika shule hiyo na amemtaka awe amezikabidhi Jumatatu  bila kukosa.

"Nimemuagiza DED (mkurugenzi) atoe Sh7 milioni kati ya Sh42 milioni za mfuko wa Jimbo nilizozizuia ziende kutatua changamoto ya choo kwenye hiyo shule na amenihakikishia zitaenda Jumatatu," amesema Sabaya.

Shule hiyo haina choo cha walimu kwa miaka 10 sasa na walimu wamekuwa wakijisaidia katika choo cha Zahanati iliyopo jirani na shule jambo ambalo Sabaya amesema halikubaliki na ndio maana ameelekeza sehemu ya fedha za mfuko wa Jimbo ziende huko.

Tayari Halmashauri ya wilaya ya Hai kupitia kwa mkurugenzi wake Sintoo imekabidhi mifuko 20 ya Saruji kwa ajili ya kuanzisha mchakato huo na ndipo Sabaya alipoingilia kati ili choo hicho kijengwe na kukamilika Januari 2020.

Jitihada za kumpaka Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema kuzungumzia uamuzi huo wa Sabaya zinaendelea.