Shirika la Elimu Kibaha lawatunukia tuzo viongozi wa Tanzania

Muktasari:

Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1963 na alilikabidhi Serikalini mwaka 1970 na limeendelea kuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya elimu katika Mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.          

Pwani. Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete wametunukiwa tuzo ya heshima na Shirika la Elimu Kibaha (SEK) ikiwa inaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa SEK, Robert Shilingi amesema tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wa wadau hao katika maendeleo ya shirika hilo ambalo lilianzishwa na Mwalimu Nyerere 1963 na kukabidhiwa kwa Serikali mwaka 1970.

Wengine waliopata tuzo hiyo ni Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hayati Ferdinand Swai hayati Bertil Merlin kutoka nchini Sweden ambaye alikuwa Mkurugenzi wa kwanza wa shirika hilo.

Watu wengine waliopata tuzo hizo ni pamoja na Profesa Philemon Sarungi ambaye ni mmoja wa wataalamu bingwa wa mifupa nchini na aliwahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri wa Afya, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Mbunge wa Rorya.

Shirika hilo limekuwa msaada katika maendeleo ya elimu katika mkoa wa Pwani.