VIDEO: 20 wafariki wakigombea kupaka mafuta ya upako mjini Moshi

Moshi. Watu 20 wamekufa kwa kukanyagana katika harakati za kutaka kukanyaga mafuta ya upako kwenye kongamano la Mtume Boniface Mwaiposa lililofanyika uwanja wa Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Tukio hilo baya kuwahi kuukumba mkoa wa Kilimanjaro limetokea leo jioni Jumamosi Februari Mosi, 2020.
Habari zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa watu zaidi ya 40 walikanyagana katika harakati hizo na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
Idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka  kwa kuwa hakuna taarifa ya ujumla ya majeruhi waliopelekwa katika vituo vya afya vya jirani pamoja na Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Awali,   kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni amesema  hakuwa na taarifa za tukio hilo lakini baadae alipotafutwa  simu yake iliita bila majibu.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba amelithibitishia Mwananchi leo  saa 5:00 usiku kuwa taarifa za awali waumini 20 wamekufa lakini akasisitiza hizo ni taarifa za awali.
“Taarifa za awali tulizonazo ni kuwa ni waumini 20 wamepoteza maisha lakini tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kama kuna watu walipelekwa huko,” amesema Kippi.
Taarifa zaidi zaidi za tukio hilo zinadai waumini hao walikumbwa na maafa hayo wakati wakikanyagana kwa ajili ya kugombania kukanyaga mafuta yaliyomwaga na mhubiri huyo yakidaiwa kuwa na upako.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi