Mwakilishi kuwasilisha hoja iliyoshtukiwa na Maalim Seif

Unguja. Mwakilishi wa Shaurimoyo (CCM), Hamza Hassan Juma amesema kesho atawasilisha hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi akitaka wanaojiunga na vyama kutoruhusiwa kugombea urais, uwakilishi na udiwani Zanzibar kabla ya kutimiza miaka miwili tangu walipojiunga.

Uamuzi huo umekishtua chama cha ACT-Wazalendo ambacho kimesema kitapinga sheria hiyo mahakamani endapo itapishwa kwa kuwa inakiuka misingi ya katiba, demokrasia na utawala bora.

Endapo hoja hiyo itapitishwa na kutungwa sheria huenda ikawa kitanzi kwa mshauri wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake ambao Machi 18, 2019 walihama CUF na kujiounga chama hicho.

Maalim Seif na timu yake walijiunga na ACT wakipinga uamuzi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF.

Jana, Juma akizungumza na Mwananchi alisema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kushaurina na wananchi wa jimbo lake na kuona kuna kila sababu ya kuifikisha hoja hiyo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi ulioanza jana.

Alisema kwa kuwa wapinzani walisusa uchaguzi wa m,arudio na hivyo CCM ikawa na wawakilishi wengi kwenye Baraza hilo, watakuwa na jukumu la kumuunga mkono na kuipitisha.

Hata hivyo, mwakilishi huyo alisema hoja yake hailengi kumzuia Maalim Seif wala wafuasi wake pekee, bali hata wanachama wanaohamia CCM.

“Kwa mfano leo hii chama cha CUF kina wabunge wengi, lakini baada ya Bunge kuvunjwa wote watageuka na kuwa ACT-Wazalendo, jambo ambalo kiuhalisia halipo sawa,” alisema.

Hoja ya mwakilishi huyo ilipingwa na Omar Said Shaaban, mwenyekiti wa kamati ya katiba na sheria wa ACT-Wazalendo, akisema inakiuka misingi iliyowekwa na katiba, hivyo chama hicho kitaipinga mahakamani.

Alisema ni wazi kwa kuwa sheria hiyo inakiuka misingi ya kikatiba ACT-Wazalendo haitakubaliana nayo.

“Na katika hili nimwombe kaka yangu mwanasheria mkuu asikubali kushawishiwa na wawakilishi hawa na kuingia kwenye mtego wa kupeleka mabadiliko hayo Barazani, kwa kuwa ataingia kwenye rekodi mbaya sana,” alisema.

“Naomba niwaambie CCM kuwa mpango wanaotaka kuutekeleza utakuwa ni kituko na wanahitaji kuutafakari mara mbili kabla ya kuibua hoja hiyo barazani,” aliongeza.