Majaliwa ataka umakini utoaji vitambulisho vya Taifa mipakani

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji kuwa makini katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwenye Mikoa ya mipakani.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji kuwa makini katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwenye Mikoa ya mipakani.

Amesema lengo si kumkomoa mtu bali kuimarisha usalama wa nchi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo muda mchache baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wabunge wa Mkoa wa Kagera kuhusu usumbufu wanaoupata wananchi wanaofuatilia vitambulisho vya Taifa huku wengine wakidaiwa kuwa si  raia.

Malalamiko hayo yametolewa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera. Majaliwa ni mlezi wa CCM mkoani Kagera.

“Watu wafuate taratibu katika suala la ugawaji wa vitambulisho, Idara ya uhamiaji wafuatilie kwa umakini kwa sababu lazima usalama wa nchi usimamiwe ipasavyo hususani katika mikoa ya mipakani.”

“Watanzania mnatakiwa muwe makini msiruhusu watu kuingia kwa njia za panya kwani watu hao hawana nia njema,” amesema Majaliwa

Majaliwa alitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wakazi wa eneo hilo kwa kuwaambia kuwa zoezi hilo lazima lifanyike kwa ufasaha na haraka ili wananchi waweze kupata vitambulisho.

“Tayari Serikali imeshaongeza vifaa na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa,”

Majaliwa alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi na wanachama wa CCM kuimarisha mshikamano miongoni mwao na pale kwenye dosari zirekebishwe kwa sababu hakuna jambo lisiloweza kutatuliwa.

“Tunahitaji kuwa na umoja na mshikamano ndani ya chama ili sote kwa pamoja tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea. Hata katiba yetu ya chama inatuhimiza tushikamane kwani wote tunajenga nyumba moja hivyo hatuna sababu ya kugombea fito,” amesema Majaliwa.

Amesema lazima viongozi hao wahakikishe kuwa CCM kinabaki salama na kinaendelea kushika dola.

“Ni wajibu wa kila kiongozi na mwanachama kuwezesha malengo hayo kutimia na ni lazima kila tawi litafakari namna ya kukiwezesha chama kujitegemea kiuchumi.”

 “Lakini pia mjiepushe na ukabila na udini katika kuteua mtu wa kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hiki na badala yake mteue mtu ambaye anauzika ndani na nje ya chama,” amesema Majaliwa