Swizz Beats aipaisha singeli kimataifa

Muktasari:

Siku moja baada ya mtayarishaji wa muziki nchini Marekani, Swizz Beats kuomba wimbo Gere wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz leo Alhamisi Februari 20, 2020 ameweka kwa mara ya pili katika ukurasa wake wa Instagram wimbo wa singeli unaoitwa Wanga.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya mtayarishaji wa muziki nchini Marekani, Swizz Beats kuomba wimbo Gere wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz leo Alhamisi Februari 20, 2020 ameweka kwa mara ya pili katika ukurasa wake wa Instagram wimbo wa singeli unaoitwa Wanga.

Wimbo huo uliotoka takribani siku tano zilizopita imeimbwa na msanii Meja Kunta aliyemshirikisha Lavalava wa lebo ya WCB  ambayo mkurugenzi wake ni Diamond.

Jana Jumatano Februari 19, 2020 Beats aliuweka wimbo huo katika ukurasa wake huo, leo akaweka wimbo wa Gere na kisha kurudia kuweka kipande cha wimbo wa Wanga.

Baada ya kuweka nyimbo hizo, wasanii wa WCB akiwemo Mbosso amesema, “singeli imeenda bila viza Marekani.”

Wakati Mbosso akieleza hayo, Diamond amesema hiyo ndio maana ya kupeleka singeli kimataifa.

Beats ambaye jina lake halisi ni Kasseem Dean  ni mume wa msanii Alicia Keys.

Ameshawatengenezea nyimbo wanamuziki maarufu  nchini Marekani akiwemo Beyonce katika wimbo wa Check on It na Ring the Alarm.

Nyimbo nyingine alizozitengeneza ni Jigga My Nigga na  Girl's Best Friend  za Jay-Z; Ultralight Beam wa Kanye West;  Touch It wa Busta Rhymes; Party Up (Up in Here) wa  DMX na Gotta Man wa Eve E.