Sh340 bilioni kutumia ujenzi wa barabara Kigoma

Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale akizungumza katika utiaji saini wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 260 ya Kabingo, Kasulu na Manyovu

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Isack Kamwelwe amesaini mkataba wa ujenzi wa  barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu kwa kiwango cha lami.

Kigoma. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Isack Kamwelwe amesaini mkataba wa ujenzi wa  barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu kwa kiwango cha lami.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 260 itajengwa kwa  miaka mitatu na kugharimu Sh340 bilioni.

Akizungumza kuhusu ujenzi huo leo Alhamisi Februari 21, 2020 mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale amesema mradi huo utachochea maendeleo na uwekezaji ndani na nje ya Tanzania.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuza biashara baina ya Tanzania na nchi za jirani zinazozunguka mkoa huo ikiwemo nchi ya Demokrasia ya Jamhuri ya Congo  (DRC) na Burundi.

Barabara hizo zitakazounganisha wilaya za mkoa wa Kigoma, kupitia Kasulu hadi Manyovu Wilaya ya Buhigwe yenye urefu wa kilomita  68.25,  Kanyani -Mvugwe wilayani Kasulu yenye urefu wa kilomita  70.5 , Mvungwe -Nduta wilayani Kibondo yenye urefu wa  kilomita 59.35 na Nduta-Kibondo hadi Kabingo wilayani Kakonko yenye  urefu wa kilomita  62.5.

Amesema mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa mkopo nafuu  wa Sh340 bilioni.